FOMU za mbio ndefu za
Uhuru, maarufu kama Uhuru Marathon, zinatarajiwa kuanza kutolewa kesho
Jumatano, huku Watanzania wakiombwa wachangie kwa gharama ndogo.
Akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon,
Innocent Melleck alisema, katika kuhakikisha kila mtu anashiriki kutakuwa na
vituo 13 vitakavyofunguliwa kwa ajili ya kutoa fomu hizo, huku pia kukiwa na
watu maalumu watakaozisambaza maofisini na hata majumbani.
Melleck alisema, fomu hizo
zitatolewa kwa Sh 100,000 kwa wale watakaotaka kukimbia mbio za kilomita tatu,
Sh 2,000 mbio za kilomita tano, Sh 6,000 kwa atakayeshiriki moja kati yam bio
za kilomita 21 au 42.
“Hizi mbio ni muhimu zaidi
kwa ajili ya Taifa letu, hivyo ni vyema kwa Watanzania wote wakashiriki ili
kuipigania amani iliyopo nchini mwetu.
“Tunataka kuungana na Rais
Jakaya Kikwete katika kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kuleta umoja, amani na
mshikamano ndani ya Tanzania na ndilo lengu la mbio hizi.
“Bado tunaendelea kuwaomba
wadhamini wajitokeze kuzidhamini, kwani nafasi bado ipo wazi na watambue hata
wao ni sehemu ya kupigania amani ya taifa letu,” alisema Melleck.
Katika mbio hizo,
zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali, zitakuwepo pia mbio za kilomita
3, kilomita 5, Half Marathon kilomita 21 pamoja na Full Marathon yenyewe
kilomita 42.
Mratibu huyo anasema mbio
za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada mbalimbali,
wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia kwa
ajili ya watu wa mahitaji ya aina mbalimbali.
“Hapa tunachotaka kufanya
katika mbio za kilomita 3 ni kuwaomba kama vile viongozi maarufu wa dini
mbalimbali pamoja na viongozi wetu ili kushiriki, kwa kudumisha amani na
upendo.
“Pia tutahakikisha kama
mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia watu wenye mahitaji
mbalimbali na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha maarufu zaidi duniani
kushiriki,” anasema.
Mratibu huyo anafafanua
kuwa wamejipanga mno katika hilo ili kuhakikisha wanafanya mambo makubwa zaidi
na ambayo yataleta tija kwa taifa.
0 comments:
Post a Comment