Kiongozi wa
Mbio za Mwenge taifa Juma Ali Simai akimkabidhi Mwenge wa Uhuru mkimbiza mwenge namba moja katika manispaa ya
Lindi Mke wa Rais ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) Mama
Salma Kikwete wakati mwenge huo ulipowasili leo katika eneo la Mto Mkavu –
Mbanja. Wapili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Lindi Dk. Mohamed Nassor.
********
Na Anna Nkinda – Maelezo,
Lindi
Vijana nchini wametakiwa kuwa
wawazi, waaminifu na waadilifu kwani huo ndiyo msingi mkubwa wa kupambana na
rushwa ili waweze kuwa viongozi wazuri hapo baadaye.
Rai hio imetolewa leo na
Kiongozi wa Mbio za Mwenge taifa Juma Ali Simai wakati akiongea na wanafunzi wa
chuo cha ufundi cha Veta likichopo katika Manispaa ya Lindi mara baada
kuzindua klabu ya kupinga rushwa chuoni hapo.
Alisema kuwa hivi sasa kuna
baadhi ya viongozi ambao wanakusanya mapato na kodi za wananchi na kuzitumia
vibaya na hivyo kusababisha shughuli za maendelea kutofanyika ikiwa ni
pamoja na kutojengwa kwa shule na vituo vya afya na wanaoathirika ni wananchi
wote.
Simai alisema, “Vijana ni
tegemeo la taifa chukueni hatua dhidi ya rushwa, kila mtu awajibike kwa
kutoa taarifa na ushahidi ili wahusika wachukuliwe hatua ni lazima
mjifunze kutokana na makosa yanayofanyika leo ili nanyi msifikie huko kwani
rushwa ni mbaya na adui mkubwa wa maendeleo”
Kiongozi huyo wa mbio za
Mwenge Taifa alisema mtu ukiwa muadilifu na muaminifu hata sehemu
ya kazi utaonekana na utapanda kutoka hatua moja kwenda nyingine bila ya
kutoa rushwa na kutoa mfano kwa wanafunzi hao mara baada ya kumaliza masomo yao
watapata ajira bila ya kutoa rushwa kwani ni haki yao kuajiriwa au
kujiajiri.
“Kama wananchi watapata
taarifa na haki zao kwa wakati kutoka kwa viongozi wao wataepukana na
mazingira ya rushwa lakini hivi sasa kuna baadhi ya watu wanaona kuwa
hawawezi kupata haki zao za msingi hadi watoe rushwa.
Ninawaomba wale wote wenye
tabia hii muiache na mtoe taarifa kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(TAKUKURU) ili pale mnapoombwa kufanya hivyo kwani rushwa ni adui wa haki na
mfahamu kuwa kwa anayetoa na anayepokea wote wanakabiliwa na kosa la jinai”,
alisema Simai.
Simai alisema kuwa ni muhimu
vijana wakawajibika na kuwa wawazi katika mambo wanayoyafanya kwa maana
ya kwamba wakipata nafasi wawashirikishe na wengine pia wafuate misingi
ya utawala bora katika kupambana na rushwa.
Akisoma taarifa ya klabu ya
wapinga rushwa katika chuo hicho Christina Mkolela ambaye ni mwanachama alisema
kuwa ili kupambana na rushwa katika halmashauri ya Manispaa ya Lindi waliamua
kuanzisha klabu hiyo ikiwa ni moja ya mkakati wa kuelimisha vijana waliopo
vyuoni ili kuwajengea uzalendo wa kuchukia rushwa na baadaye kuwa raia wema
wasiopenda kupokea wala kutoa rushwa.
Alisema klabu hiyo ilianzishwa
mwaka 2013 ikiwa na wanachama 91 kati ya hao wasichana ni 21 na wavulana ni 70
ambao wanashiriki katika kutoa elimu ya kuzuia na kupambaa na rushwa kwa
wenzao.
Mkolela alisema, “Klabu hii ni
ya kudumu na itaendelea kupokea wanachama ambao ni wanavyuo watakaokuja chuoni
hapo kila mwaka na hivyo kuifanya kuwa endelevu”.
Kabla ya kuwasili chuoni hapo
Mwenge huo wa uhuru ulipokelewa kutoka wilaya ya Lindi na viongozi wa
Serikali na vyama vya siasa wa Manispaa ya Lindi akiwemo mke wa Rais Mama Salma
Kikwete katika eneo la Mto Mkavu – Mbanja.
Ukiwa katika Manispaa ya Lindi
Mwenge wa uhuru utafungua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba
ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kati ya miradi hiyo ni mradi
wa maji safi kwa matumizi ya binadamu na mradi wa samaki.
Sherehe za kilele za
mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitaenda sambamba na kumbukumbu ya kifo
cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na maadhimisho ya wiki ya
vijana zinatarajia kufanyika tarehe 14/10/2013 katika uwanja wa Samora uliopo
Manispaa ya Iringa.
0 comments:
Post a Comment