Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Vilevile Kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa (Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo hazikuafikiana.
UCHAGUZI TFF SASA KUFANYIKA OKTOBA 27
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo katika kifungu cha 10(6) cha Kanuni za Uchaguzi za TFF inasogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa TFF kutoka Oktoba 20 mpaka Oktoba 26 na 27 mwaka huu.
Sababu za kusogeza mbele uchaguzi ni kutokana na ukweli kuwa Oktoba 20 mwaka huu uongozi wa TFF utakuwa na shughuli nyingi za maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga, na hivyo haitawezekana kusimamia shughuli za Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kwa wakati mmoja na mchezo huo.
Siku ya mwisho ya kampeni itakuwa Oktoba 25 mwaka huu. Ukiondoa mabadiliko hayo ya tarehe ya uchaguzi wa viongozi wa TFF, ratiba ya mchakato wa uchaguzi na itabaki kama ilivyotangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika mkutano wake na waandishi wa habari Agosti 24 mwaka huu.
Pia Kamati imeamua kuwa uchaguzi wa Bodi ya Ligi utabakia kuwa Oktoba 18 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Kamati imesema inaamini wahusika wote watapokea vizuri mabadiliko hayo na inasikitika kwa usumbufu utakaosababishwa na mabadiliko hayo.
0 comments:
Post a Comment