Nafasi Ya Matangazo

August 20, 2013

 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara akimkabidhi Tuzo ya Ben TV Diplomatic Awards-2012  Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA, na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ofisini kwake tarehe 19.8.2013. Tuzo hiyo ilitolewa kwa Mama Salma baada ya kuibuka mshindi miongoni mwa mataifa ya bara la Afrika, Caribean, Asia na Pacific kutokana na kazi za kuendeleza rasilimai watu hapa Tanzania.
************
Na Anna Nkinda – Maelezo
19/8/2013 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya kimataifa  ya jitihada za kuendeleza rasilimali watu katika taifa kwa mwaka 2012 na Taasisi ya Bright Entertainment Network (BEN) ya nchini Uingereza.
 
Tuzo hizo pamoja na cheti amekabidhiwa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.
 
Waziri Dk. Mukangara alikabidhiwa tuzo hiyo na Taasisi ya BEN mwezi wa sita mwaka huu alipokuwa nchini Uingereza kwa shughuli za kikazi ili aifikishe kwa  Mama Kikwete.
 
Dk. Mukangara  alisema kuwa tuzo hiyo ambayo inafahamika kwa jina la “Country Human Development – 2012 Award” inatolewa kwa mshindi anayeteuliwa na Taasisi ya BEN ikiwa ni miongoni mwa waliowania kutoka nchi za Bara la Afrika , Carribbia, Asia na Pasifiki.
 
“Ushindi huu wa kimataifa Mama Kikwete umeupata kutokana na juhudi na harakati zako za kuwainua kimaendeleo wananchi wa matabaka mbalimbali hapa nchini hasa wasichana na kina mama kupitia Taasisi uliyoiasisi na kuendelea kuiendesha ya WAMA.
 
Sote tunakubalina kutokana na kazi tunazozishuhudia ambazo Taasisi yako chini ya uongozi wako inazifanya, hakika umestahili kutunukiwa tuzo hii ya jitihada za kuendeleza rasilimali  watu katika taifa hongera sana”, alisema Waziri Dk. Mukangara.
 
Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alimshukuru waziri Dk. Mukangara kwa kuchukua dhamana ya kupokea tuzo hiyo na kuifikisha kwake pia aliishukuru Taasisi ya BEN kwa kuona umuhimu wa kazi anazozifanya na kumchagua kuwa mmoja wa washindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2012 kwani watu walioshiriki ni wengi kutoka ndani na n je ya bara la Afrika.
 
“Ninashukuru sana kwa tuzo hii niliyoipata ambayo inazidi kunipa moyo na ninaahidi nitaendelea kufanya kazi kwa kujituma kadri Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha na sintarudi nyuma kuwasaidia watanzania eti kwa kuwa nimepata tuzo kwani  sikutegemea kuwa ipo siku nitapata tuzo kutokana na kazi ninazozifanya za kuisaidia jamii”.
 
Hii tuzo ni kwa ajili ya  watanzania wote na wafanyakazi wa taasisi ya WAMA kwani bila ya watanzania nisingeweza kupata tuzo kama hii”, alisema Mama Kikwete.  
 
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema taasisi zote za maendeleo zitaendelea kufanya kazi kwa bidii ili ziweze kutimiza malengo ya Maendeleo ya Milinia kwa wakati uliokusudiwa.
 
Kazi zinazofanywa na Taasisi ya WAMA zilizopelekea Mwenyekiti wa Taasisi hiyo kupewa tuzo ni uraghibishi wa kuboresha hali ya maisha kwa watoto, wasichana na wanawake hasa kwa upande wa afya, elimu na uchumi na kuwasaidia mitaji kinamama wajasiriamali.
 
Zingine ni kupambana na mimba za utotoni hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari  na kuendesha  mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kina mama, hususani kupunguza maambukiziya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Posted by MROKI On Tuesday, August 20, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo