Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, akisoma hotuba yake hii leo.
Mheshimi wa Shamsi Vuai Nahodha
(Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa;
Mheshimiwa Gril Haskel, Balozi wa
Israel;
Meja Jenerali Raphael Muhuga,Mkuu
wa Jeshi la Kujenga Taifa,
Makamanda, Wapiganaji na Vijana;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Historia ya JKT
Ndugu Wananchi;
Miaka 50 iliyopita, tarehe kama ya
leo, yaani tarehe 10 Julai, 1963 Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa rasmi. Huu ulikuwa ni utekelezaji wa Azimio la Kikao
cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika tarehe 19 Aprili, 1963 chini ya uongozi
wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika. Wazo la kuanzishwa kwa JKT lilitokana na mapendekezo ya busara
ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU Youth League), uliofanyika
mkoani Tabora mwaka 1958. Wazo hili
lilitolewa na Katibu Mkuu wa TANU Youth League wakati ule Ndugu Joseph Nyerere ambaye
sasa ni marehemu. Lengo kuu la kutaka kuundwa
kwa JKT lilikuwa ni kuwandaa vijana kuwa raia wema, wawe na moyo wa uzalendo,
na wawe tayari kulitumikia taifa lao kwa nguvu na uwezo wao wote.
Ndugu Wananchi;
Jeshi la Kujenga
Taifa lilianza na Vijana 11 kutoka Wilaya 11 nchini. Hao ndio walikuwa wa kwanza kupata mafunzo
katika Kambi ya JKT Mgulani, Jijini Dar es Salaam. Vijana hao walikuwa ni Makatibu wa Umoja wa
Vijana wa TANU na wengine walimu. Niruhusuni
niwatambue watu hao kuwa ni Bi Zainabu Kiango, Bw. Sebastian Chale, Bw. Peter
Lwegarulira, Bw. Rupho Kamba, Bw. Hashim Ngaliwason, Bw. John Ndimugangwo, Bw.
Said Desai, Bw. Dismas Msilu (Brigedia Mstaafu), Bw. Athumani Msonge (Brigedia
Jenerali Mstaafu), Bw. Reginald Mitande na Bw. Eslei Mwakyambiki.
Kati ya hao 11, walio hai ni Bi Zainabu Kiango na Brig. Jenerali Dismass Msillu
ambao wapo nasi siku ya leo. Waliosalia
wameshatangulia mbele ya haki. Mwenyezi Mungu
awarehemu. Kundi la pili liliwajumuisha Bi.
M. Mhando, Bw. E. Simkone, Bw. Mwanimlele (Asst Master) Bw. AA Moyo (Asst
Master) ambao walijiunga na kupata mafunzo ya uongozi.
Sheria Iliyoanzisha JKT
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1964, Bunge lilitunga Sheria ya
Kuanzisha JKT iliyoupa nguvu ya kisheria uamuzi wa mwaka 1963 wa Baraza la
Mawaziri wa kuanzishwa kwa Jeshi hilo.
Kwa mujibu wa Sheria ile, kujiunga na JKT ilikuwa jambo la kujitolea kwa
mapenzi ya mtu. Lakini mwaka 1966, Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuanzisha
utaratibu wa kujiunga na JKT kwa mujibu wa Sheria.
Utaratibu huu uliwahusu vijana waliohitimu vyuo vikuu, vyuo vya elimu ya
juu, kidato cha sita na waliomaliza kidato cha nne ambao wamepata mafunzo
kwenye vyuo vya taaluma mbalimbali kama vile ualimu, uganga, uuguzi na
kadhalika. Mkurugenzi wa JKT aliwezeshwa kisheria kuwaita
vijana hao kujiunga na JKT. Mwezi Julai
1967, kikundi cha kwanza cha vijana wasomi 64
kilijiunga na JKT katika
Operesheni
Azimio.
Katika kuunga mkono
uamuzi wa Serikali kuhusu kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa, viongozi na
wasomi wengine waliohitimu zamani waliamua kujiunga na mafunzo ya JKT. Mwezi Januari, 1968, kwa mfano, aliyekuwa
Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Rashid Kawawa, aliyekuwa Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Aboud Jumbe, aliyekuwa Spika wa
Bunge Chifu Adam Sapi Mkwawa pamoja na baadhi ya Wabunge na viongozi mbalimbali
wa Chama na Serikali walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa. Wote walikuwa katika kambi ya Ruvu ambapo
walipatiwa mafunzo ya uongozi.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1975 JKT iliunganishwa na Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na hivyo kuwa sehemu kamili ya JWTZ. Kuanzia wakati ule, Maafisa na Askari wa JKT
wakawa ni wa JWTZ na kutambulika kwa vyeo vya JWTZ. Jeshi la Kujenga Taifa liliendelea na
majukumu yake ya kutoa mafunzo kwa vijana wa kujitolea na wa mujibu wa
sheria. Hata hivyo, mambo mawili ya
msingi yalisisitizwa au kuongezwa katika majukumu ya JKT. Kwanza kwamba, kuwa Divisheni ya Uzalishaji
ya JWTZ yenye dhamana ya kulipatia Jeshi mahitaji yake ya chakula, mavazi na
mengineyo. Pili, kwamba JKT ndipo mahali
pa kutolea mafunzo ya awali ya kijeshi na kwamba JWTZ itaajiri kutokana na
wanaohitimu JKT.
Katika dhamira ya kutimiza wajibu wa
kwanza kwa ufanisi, mwaka 1982 Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT)
liliundwa. Shabaha kuu ilikuwa ni kuwa
na chombo madhubuti cha kupanga, kusimamia, kuratibu na kutekeleza majukumu ya
uzalishaji mali na kiuchumi katika JKT kazi ambayo shirika linaendelea kuifanya
hadi sasa.
Kusitishwa kwa Mafunzo ya JKT
Ndugu
Wananchi
Tunapoangalia
nyuma, katika historia ya miaka 50 ya kuzaliwa na uhai wa JKT tunaona wazi kuwa
yamepatikana mafanikio makubwa. Tena ni
mafanikio ya kutia moyo na kujivunia.
Ninaposema hivyo, napenda nisieleweke vibaya kuwa sitambui ukweli kwamba
kulikuwepo vipindi vigumu vyenye changamoto za namna mbalimbali. Zilikuwepo changamoto kubwa na ndogo na
zilizokuwa ngumu na nyepesi kuzipatia ufumbuzi.
Aidha, natambua kuwa bado zipo changamoto kadhaa tunazoendelea kukabiliana
nazo. Jambo la msingi na la faraja ni
kwamba pamoja na changamoto hii tumefanikiwa sana.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
upande wa mafunzo kwa vijana, kwa mfano, zaidi ya vijana 305,625 wamepitia JKT na kupatiwa mafunzo ya kijeshi na ya stadi
mbalimbali za maisha katika fani na nyanja mbalimbali. Tangu mwaka 1963 mpaka sasa yameshapita
makundi (kwa jina maarufu Operesheni) 102.
Bahati
mbaya kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi iliyoikabili nchi yetu kuanzia nusu ya
pili ya miaka ya 1970 na kuwa mbaya zaidi miaka ya 1980 na mwanzoni mwa 1990,
hali ya utoaji wa mafunzo kwa vijana katika JKT iliathirika sana. Upatikanaji wa huduma na mahitaji kwa ajili
ya mafunzo na kuendesha kambi na JKT kwa jumla ukawa mgumu.
Pengine
ni vyema nikaeleza kuwa kupanda sana kwa bei ya mafuta duniani, kuanguka kwa
bei za mazao yetu tunayouza nje na gharama kubwa ya vita dhidi ya Idi Amin wa
Uganda ndivyo vilivyosababisha uchumi wa nchi yetu kutetereka. Hali
hii ilipunguza sana uwezo wa Serikali kutimiza majukumu yake ya msingi katika
sekta, karibu zote nchini.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
sababu hiyo, kwa upande wa JKT mwaka 1993, Serikali ililazimika kusimamisha
mafunzo kwa vijana wa kujitolea na mwaka 1994 ilifanyika hivyo kwa vijana wa mujibu
wa Sheria. Kwa kweli baada ya mwaka 1994
shughuli za msingi za JKT zilidorora sana na kubakiza za kulinda kambi na zile Shirika
la Uchumi (SUMAJKT). Hata hizo nazo hazikuwa
zinafanyika kwa kiwango kikubwa wala hazikuwa kwa ufanisi mkubwa kwa sababu ya
kutokupata fedha za kutosha kutoka Serikalini.
Fedha za uendeshaji wa shughuli zake zilikuwa kidogo.
Ndugu
Wananchi;
Kuifufua JKT ilikuwa ni moja ya
mambo niliyoyapa kipaumbele cha juu nilichojiwekea katika mipango ya kazi baada
ya kupewa heshima kubwa ya kuliongoza taifa letu Desemba 21, 2005. Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya kuzindua
Bunge tarehe 30 Desemba, 2005, nilipozungumzia kufanya kila tuwezalo kujenga
moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana, nilikuwa nazungumzia kufufua na
kuimarisha Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na kuwepo kwa shule za kitaifa hasa za
sekondari.
Ni
ukweli ulio wazi kwamba JKT imefanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga moyo wa
utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana waliopitia Jeshi hilo. Hapa ni mahali ambapo vijana wa rangi zote,
makabila yote, dini zote hukutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi
kama ndugu wa nchi moja. Hakuna chombo
chochote cha malezi ya vijana kilichoizidi JKT katika kazi hiyo. Kwangu mimi na wenzangu katika Serikali
ninayoiongoza kufufua mafunzo ya vijana wa kujitolea na mujibu wa sheria
lilikuwa suala kubwa na muhimu sana kulitekeleza.
Ndugu
Wananchi;
Bahati nzuri sikuwa peke yangu
mwenye fikira na matamanio hayo. Watu
wengi ndani ya Serikali, nje ya Serikali na miongoni mwa raia na Bungeni
walikuwa wanaunga mkono mawazo hayo. Sababu
kubwa ni kuwa athari za kusimamishwa mafunzo ya JKT ziliwagusa wengi na ndiyo
maana kumekuwepo na madai ya kutaka mafunzo yarudishwe.
Kule
Bungeni kauli yangu kuhusu JKT iligeuka kuwa deni kubwa kwangu na kwa
Serikali. Madai ya kutaka Serikali
irejeshe mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria yalikuwa yanajitokeza mara kwa
mara na mwangi wake ulikuwa unaongezeka ukali kila mwaka. Nafurahi kwamba hatimaye tarehe 26 Machi, 2013
tulifanikiwa kutimiza dhamira na ahadi yetu nilipozindua kuanza upya kwa
mafunzo hayo katika kambi ya Ruvu. Kundi
la kwanza limemaliza mafunzo yake na la pili limeshafika katika makambi na tayari
wameanza mafunzo.
Kama ilivyokuwa mwaka 1964 JKT
ilipoanza, na mwaka 1968 baada ya mafunzo ya mujibu wa Sheria kuanzishwa,
viongozi wa kitaifa waliongoza kwa mfano; safari hii Wabunge wetu alionesha. Mwaka huu Wabunge 22 wamefanya na kumaliza mafunzo ya uongozi. Baadhi yao wako nasi siku ya leo. Niruhusuni nirudie kutoa pongezi zangu za dhati
kwao kwa kuwa viongozi wa mfano.
Ndugu
Wananchi;
Taarifa
nilizonazo ni kuwa wamefanya na kumaliza mafunzo yao vizuri. Walikuwa na nidhamu nzuri, utii na moyo wa
kujituma. Wamemaliza wakiwa ni askari
wakakamavu na wenye mtazamo mpya na bora zaidi kuhusu masuala ya utaifa,
uzalendo na mustakabali wa taifa letu na watu wake.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa shughuli za kiuchumi
zinazofanywa na JKT tuliazimia kuwa, tutafanya kila tuwezalo kuimarisha
SUMAJKT. Tumefanya mambo kadhaa kwa
ajili hiyo na tumekuwa tunapata mafanikio ingawaje bado tunayo safari ndefu ya
kulijenga shirika hili mpaka liwe bora kwa shughuli lizifanyazo. Naamini tutafika pale tunapopatarajia.
Tuliamua kutoa upendeleo maalum kwa JKT kwa
kutoa shughuli na miradi kadhaa ya Serikali waitekeleze wao. Kwa mfano, ujenzi wa nyumba na majengo kadhaa
ya Serikali pamoja na ujenzi wa barabara, mabwawa ya maji na miradi ya kilimo
cha umwagiliaji na kadhalika. Tumewapa JKT
kazi ya kuzalisha mbegu bora kwa wakulima.
Vile vile, Serikali imechukua mkopo wa dola za Marekani milioni 40 kutoka Serikali ya India uliotumika
kununua matrekta 1,846 kutoka
Serikali ya India na kuipa SUMAJKT kuuza kwa wakulima kama biashara yao.
Hivi
sasa mchakato unaandaliwa wa kupata mkopo mwingine wa dola za Marekani milioni 92 kwa ajili hiyo. Tumefanya yote hayo kwa makusudi
mazima ya kuliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kuwa na shirika lililoimara na
linalotekeleza kwa ufanisi majukumu yake.
Halikadhalika itawezesha JKT kudumisha sifa yake nzuri katika kilimo,
ufugaji, uvuvi na ujenzi.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii, kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu, Wakuu wa JKT kumi, waliotangulia
pamoja na Meja Jenerali Muhuga aliyepo sasa.
Tunawapongeza kwa utumishi wao uliotukuka na moyo wao wa upendo kwa nchi
yetu na watu wake. Mafanikio haya tunayojivunia leo yametokana na
juhudi kubwa za viongozi hawa wakishirikiana na maafisa, askari na wafanyakazi
raia katika kubuni na kusimamia utekelezaji wa shughuli za JKT.
Mimi
na Watanzania wenzangu wote hatuna neno lingine zuri la kuwaonesha upendo wetu
na shukrani zetu zaidi ya kusema asanteni sana.
Tunatambua na kuthamini mchango wenu.
Tutauenzi daima.
Changamoto
na Dira
Mheshimiwa
Waziri;
Pamoja na mafanikio ya
kutia moyo, naelewa kuwa bado safari iliyo mbele yetu ni ndefu na imejawa na
changamoto nyingi ambazo hatuna budi kuzipatia majawabu. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na uhaba
wa makazi ya maafisa na askari, upungufu wa wataalamu katika miradi mbalimbali,
upungufu wa vitendea kazi na vyombo vya usafiri. Baadhi ya makambi hayana miundombinu mizuri ya
kutoa kwa uhakika huduma muhimu kama vile maji, umeme na kadhalika.
Napenda
kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na JKT katika kutafuta njia
mbalimbali za kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo. Tutaendelea kuongeza bajeti ya JKT kila mwaka
na kuidhamini SUMAJKT ipate mikopo ya kutekeleza miradi yake na shughuli
zake. Tutaendelea kutoa upendeleo kwa
Jeshi na JKT katika kutekeleza baadhi ya miradi ya Serikali. Hata hivyo, nawaomba mzingatie ubora wa kazi
muifanyayo ili kulinda heshima ya JKT na
kutulinda sisi tunaoamua kuwapa upendeleo.
Ndugu
Wananchi;
Tunafanya
haya kwa dhamira moja kubwa ya kutaka kulifufua Jeshi la Kujenga Taifa na
kulifikisha mahali panapostahili na kuwa chombo madhubuti cha kutumainiwa na
taifa. Nataka JKT liwe Jeshi la kisasa
zaidi, linaloenda na wakati na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya
juu. Tunapenda mafunzo yanayotolewa kwa
vijana wanaojiunga na JKT yaendeshwe vizuri.
Tunataka JKT itoe wazalendo wa kweli, wanaothamini utaifa, umoja na
mshikamano wa Watanzania. Vijana
wanaopenda kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea. Tunataka JKT izalishe askari walio hodari na wanaoweza
kulinda nchi yao kwa ujasiri mkubwa.
Aidha, wanapoajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama na kwingineko,
idhihirishe wazi kuwa vijana waliopitia JKT ni bora. Ni watu walioiva, wa kuaminika na
kutumainiwa.
Hali
kadhalika, kwa wale wanaorudi uraiani kufanya shughuli nyingine wawe ni watu
waliokamilika na wenye uwezo wa kusimama wenyewe na kuendesha maisha yao. Kinachotakiwa ni kuwepo kwa utaratibu mzuri
kuwasaidia wanaojiajiri waweze kuanzisha shughuli za kuwaingizia mapato kwa
kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata.
Namna ya kuwawezesha vijana wanaomaliza JKT waanze maisha ya kujitegemea
ni jambo ambalo hatuna budi kulitafakari.
Lakini leteni mapendekezo yenu tuone namna ya kuyatekeleza.
Ndugu
Wananchi;
Mpaka
sasa bado JKT haijafanikiwa ipasavyo kuwa divisheni ya uzalishaji ya JWTZ kama
ilivyotarajiwa. Bado haizalishi chakula cha
kutosheleza mahitaji ya JWTZ. Aidha,
bado hawajaweza kutosheleza mahitaji mengine ya JWTZ kama vile mavazi na
kadhalika. Sasa wakati umefika wa kujipanga
vizuri kutekeleza jukumu hilo. JKT
itumie sherehe hizi kufunga nadhiri ya kupanga na kuanza safari ya dhati ya kufanya
hivyo. Lakini, wasiishie hapo tu, JKT iweke
nia ya kuzalisha ziada ya kuuza nchini na hata nje ya nchi. Inawezekana, jipangeni vizuri ili mtimize wajibu
wenu.
Pongezi
Nakushukuru
sana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha
na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Raphael Muhuga kwa kunishirikisha
kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhai wa Jeshi la Kujenga Taifa. Nawapongeza sana kwa maandalizi mazuri ya
sherehe hizi ambazo hakika zimefana sana.
Gwaride lilikuwa zuri na tumeburudika vya kutosha kutoka vikundi vya
ngoma, ngonjera na nyimbo.
Kwa
niaba yangu, ya Serikali na ya Watanzania wote nawapongeza kwa dhati Maafisa
Wakuu, Maafisa Wadogo, wapiganaji na vijana wa JKT popote pale walipo kwa kusherehekea
Jubilei ya Dhahabu ya uhai wa JKT.
Mnastahili kuwa na furaha na kusherehekea kama tulivyoshuhudia sote.
Rai kwa
Makamanda wa JKT
Ndugu
Mkuu wa JKT, Makamanda, Maafisa na Askari;
Ni jambo linalotia faraja
kubwa kwamba sote tunatambua kuwa katika miaka 50 iliyopita Jeshi la Kujenga
Taifa limepata mafanikio ya kutia moyo ingawaje safari ilikuwa na vikwazo
mbalimbali. Hata huko mbele muendako hatutegemei
kuwa mambo yatakuwa rahisi, changamoto mbalimbali zitaendelea kujitokeza. Hivyo basi, kinachohitajika ni kuendelea kuwa
wabunifu kufanya kazi ya ziada, tena kwa bidii zaidi, maarifa na moyo wa
kujituma na kujitolea. Hizi ni sifa ambazo
mnazo, hivyo naomba muendelee kuzidumisha na kuziendeleza.
Endeleeni kuwa chuo mahiri cha kuwafunda vijana
wetu wawe na moyo wa utaifa, uzalendo, kujituma na kupenda kufanya kazi. Wawe raia wema na wawe tayari kutoa mchango
stahiki katika kujenga taifa lao. JKT
inategemewa kuendelea kuwa kitovu cha shughuli za uzalishaji mali, mafunzo ya
stadi za kazi na ujasiriamali kwa vijana wetu.
Endeleeni kuimarisha JKT.
Nawaomba mtimize wajibu wenu huo kwa
ukamilifu. Msituangushe. Nawaomba endeleeni kuwa na moyo wa kuchapa
kazi, muwe makini na waaminifu katika
utendaji wenu wa kazi za kila siku.
Tafadhali zingatieni sana viapo vyenu vya utumishi jeshini kwa kila
ngazi ya uongozi. Muwe na nidhamu siku
zote kama mwanajeshi anavyotakiwa kuwa.
Mkifanya hivyo, nina imani kuwa katika miaka michache ijayo JKT itapiga
hatua kubwa ya maendeleo. Taifa
litanufaika sana.
Shukrani
kwa Israel
Ndugu
Wananchi;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitatambua na kuwashukuru marafiki zetu wa Israel. Nchi ya Israel ndiyo iliyotupatia wakufunzi
wa kwanza waliotusaidia katika kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa. Aidha, walitoa mafunzo kwa viongozi wetu
kadhaa waasisi wa JKT nchini Israel.
Serikali ya Israel imewakilishwa hapa leo na Balozi wake nchini Mheshimiwa
Gril Haskel. Naomba Balozi atufikishie
salamu zetu nyingi za shukrani kwa Rais Shimon Peres, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
na watu wote wa Israel kwa mchango wao muhimu walioutoa katika kuanzisha na
kujenga Jeshi la Kujenga Taifa.
Hatasahau kamwe.
Mwisho
Ndugu
Wananchi;
Mwisho, nawashukuru, kwa mara
nyingine tena, Mheshimiwa Waziri Shamsi Nahodha na Meja Jenerali Muhuga kwa
kunialika. Nawashukuru wananchi na viongozi
mbalimbali wa Serikali na wa vyama vya siasa kwa kuja kwa wingi kushiriki
katika sherehe za siku ya leo. Na, kwa
namna ya pekee nawashukuru wananchi wote waliotembelea maonesho ya shughuli
zinazofanywa na JKT. Mmejionea wenyewe na kusikia faida za kuwepo kwa
JKT. Basi tuendelee kuliunga mkono Jeshi
letu, lipate mafanikio makubwa zaidi miaka 50 ijayo.
Asanteni kwa kunisikiliza
0 comments:
Post a Comment