Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Azam ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa
kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Ushindi wa jumla ya mabao 8-1
ambao Azam imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu
hiyo tu, bali Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga
kiushindani katika michuano hiyo ya Afrika.
Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya
Wakurugenzi ya klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo
wakautazama ushindi huo kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri
zaidi kwa raundi inayofuata.
Timu ya Azam inayofundishwa na
Mwingereza John Stewart Hall ilishinda nyumbani mechi ya kwanza mabao 3-1, na
jana kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini jijini Juba.
Kwa kufanikiwa kuing’oa Al
Nasir Juba, Azam sasa watacheza raundi ya kwanza (raundi ya 16 bora) ya
michuano dhidi ya Barrack Y.C.II ya Liberia ambayo katika raundi ya awali
iliitoa Johansens ya Sierra Leone. Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika
mechi ya kwanza na kulazimisha suluhu katika mechi ya marudiano jijini
Freetown.
Azam itaanzia mechi hiyo
ugenini kati ya Machi 15,16 na 17 mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa
Tanzania kati ya Aprili 5,6 na 7 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment