Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari 23, 2013 kuhudhuria
utiwaji saini Mpango wa
Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
****** ******
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari
23, 2013 kuhudhuria utiwaji saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama
na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mpango huo unatarajiwa kutiwa saini kesho
Februari 24, 2013 na Wakuu wa Nchi kutoka Ukanda wa Maziwa Makuu, ikiwa ni
pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Uganda, Jamhuri ya
Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kongo
(Brazaville), Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Jamhuri ya Afrika Kusini.
Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban
Ki Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma,
pamoja na wenyeviti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Ukanda
wa Maziwa Makuu (ICGLR) watatia saini Mpango huo kama mashahidi na wadhamini.
Mpango huo una nia ya kuchangia juhudi ambazo
zimefanywa na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC) katika kutafuta amani Mashariki ya Kongo na ukanda wote wa
Maziwa Makuu kwa ujumla.
Mpango huo pia umetilia maanani mapendekezo
muhimu yaliyokubalika baada ya mashauriano kati ya wakuu wa nchi za Ukanda wa
Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
“Mwisho”
Imetolewa na:
Muhidin Issa Michuzi,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Februari, 2013
0 comments:
Post a Comment