Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye akiongea na Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba aliokutana nao leo (Alhamisi, Jan 17, 2013) kutoa
maoni yake kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji
Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu
Dkt. Salim Ahmed Salim (katikati).
Na Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya
habari yakiwemo baadhi ya magazeti ya leo (Alhamisi, Januari 17, 2013) ambazo zinaashiria
kuwa Tume inakataa kupokea baadhi ya maoni yanayowasilishwa kwake na
makundi mbalimbali.
Taarifa hizo za vyombo
vya habari zimetokana na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Ununuzi wa Umma (PPRA) Dkt. Ramadhan Mlinga aliyoitoa mara baada ya taasisi
yake kuwasilisha kwa Tume maoni kuhusu Katiba Mpya siku ya Jumatano, tarehe 16
Januari, 2013 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa
hizo, mara baada ya PPRA kuwasilisha maoni kwa Tume, Wajumbe wa Tume walisita
kupokea maoni ya taasisi hiyo na badala yake kuagiza PPRA kuandaa maoni tena na
kuyawasilisha katika Tume ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe 16 Januari, 2013.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa leo (Alhamisi, Januari 17, 2013) kwa vyombo vya habari na Katibu wa
Tume hiyo Ndg. Assaa Rashid, taarifa hizo siyo za kweli na kuwa Tume yake haina
mamlaka ya kisheria ya kukataa kupokea maoni.
“Tume inapenda kuwataarifu
wananchi, makundi, taasisi na wadau wengine wote kuwa Tume haijakataa na haina
mamlaka ya kisheria ya kukataa kupokea maoni ya mtu, jumuiya, taasisi au kundi
lolote,” alisema Ndg. Assaa katika taarifa yake na kuongeza:
“Katika mikutano
inayoendelea (na makundi mbalimbali), kabla ya kuhitimisha mkutano husika, Tume
huomba
chama cha siasa, jumuiya, taasisi au mtu aliyewasilisha maoni kutoa ufafanuzi wa
hoja mbalimbali zilizojitokeza katika kikao” alisema na kufafanua kuwa ufafanuzi
huu hutolewa kwa hiari palepale katika mkutano au kwa maandishi baada ya siku kadhaa
ambazo Tume hukubaliana na mtu au kikundi kilichowasilisha maoni.
Akifafanua zaidi Ndg.
Assaa ameseama kuwa mikutano inayoendelea kati ya Tume na
Makundi mbalimbali inafuatia kukamilika kwa mikutano
ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi tarehe 19 Disemba mwaka jana (2012).
“Kwa msingi huu, katika
mkutano kati ya Tume na PPRA uliofanyika juzi, tarehe 15 Januari, 2013, Tume iliiomba
PPRA kuangalia uwezekano wa kutoa ufafanuzi wa masuala ya ziada ambayo Tume ilitaka
kupata maoni ya kitaalamu kutoka katika taasisi hiyo,” alisema kiongozi
huyo wa Tume na kuongeza kuwa ombi kama hilo pia limetolewa kwa makundi mengine
ambayo yameshakutana na Tume kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi tarehe 1 Mei mwaka jana (2012) na wiki
iliyopita ilianza kazi ya kukusanya maoni ya makundi na watu mbalimbali kuhusu
Katiba Mpya. Mikutano hii inatarajiwa kukamilika tarehe 25 mwezi huu (Januari,
2013).
0 comments:
Post a Comment