Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodeger
Chila Tenga akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari jijini
Dar es Salaam leo, juu ya uamuzi wake wa Kutogombea tena wadhifa huo wa
juu alioutumikia kwa miaka nane.
******
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema
hatagombea tena wadhifa huo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika
Februari 24 mwaka huu.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF leo, Rais Tenga amesema
wakati anaingia kwenye uongozi mwaka 2004 ajenda ilikuwa na kuijenga TFF
kama taasisi kwa kuweka mifumo ya uendeshaji ikiwemo kutengeneza katiba
na kanuni, jambo ambalo limefanyika.
“Wajumbe
wamekuwa wakiniuliza Rais vipi? Mimi hapana. Nilishafika pale pa
kufika. Tulipoanza wakati ule ilikuwa ni kujenga taasisi. Na kazi hiyo
tumeifanya. Tulipoingia mwaka 2004 hiyo ndiyo ilikuwa ajenda,” amesema
Rais Tenga.
Amesema
walitengeneza Katiba, vyombo huru vya kufanya uamuzi, kuongeza wigo wa
wapiga kura ambapo hivi sasa kwenye mpira wa miguu hakuwezi kutokea
migogoro, hata ikitokea kuna mfumo wa kuidhibiti.
Rais
Tenga ameishukuru Sekretarieti ya TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF,
kamati za uchaguzi za wanachama wa TFF na vyama wanachama wa TFF kwa
hatua iliyofikiwa katika uchaguzi ambapo mikoa yote imekamilisha
uchaguzi na kubaki vyama shiriki pekee.
Ametoa
mwito kwa wadau kujitokeza kugombea uongozi TFF, kwani baada ya kujenga
taasisi ajenda iliyobaki ni mpira wa miguu wenyewe ikiwemo nini
kifanyika ili mpira uchezwe katika maeneo mbalimbali.
“Tumeshatengeza
mfumo, sasa ni kuangalia jinsi ya kuendeleza mpira. Changamoto ni
tufanye nini ili mpira uendelee. Tunataka watu wengine wabebe hiyo
ajenda ili tuangalie tunakwendaje mbele,” amesema.
Pia
amesema ushirikiano ambao amepata kwa wapenzi na wadau wa mpira wa
miguu ni wa ajabu. Vilevile ameishukuru vyombo vya habari, Serikali,
klabu, wadhamini na wafadhili kwa mchango wao katika uendeshaji wa mpira
wa miguu nchini.
19 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TFF
Wadau
19 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unaotarajiwa kufanyika
Februari 24 mwaka huu.
Fomu
hizo zimeanza kutolewa leo (Januari 14 mwaka huu) ambapo wawili
wamechukua nafasi ya Makamu wa Rais wakati waliobaki wanaomba ujumbe wa
Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.
Waliochukua
fomu za umakamu wa rais ni Wallace Karia na Ramadhan Nassib. Wote ni
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza muda wake.
Waliochukua
fomu za ujumbe ni Shaffih Dauda, Athuman Kambi, Hussein Mwamba, Stewart
Masima, Yusuph Kitumbo, Mugisha Galibona, Vedastus Lufano, Twahili
Njoki, Charles Mugondo, Elley Mbise, Farid Nahdi, Ayubu Nyaulingo,
Nazarius Kilungeja, Epaphra Swai, Khalid Abdallah, James Mhagama na
Selemani Bandiho.
PONGEZI UONGOZI MPYA KATAVI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Katavi (KAREFA) uliochaguliwa katika
uchaguzi uliofanyika jana (Januari 13 mwaka huu).
Ushindi
waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika
kusimamia mchezo huo mkoani Katavi.
TFF
inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya KAREFA
chini ya ukatibu wa Peter Hella aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo
uliofanyika ukumbi wa DC mjini Mpanda kwa kumshinda Emmanuel Chaula kwa
kura sita dhidi ya mbili.
Uongozi
huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha
shughuli za mpira wa miguu mkoani Katavi kwa kuzingatia katiba ya KAREFA
pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia
tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KAREFA na Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi
waliochaguliwa ni Hella (Katibu), Elias Mande (Mjumbe wa Mkutano Mkuu
TFF) na Deo Bakuba (Mwakilishi wa Klabu TFF). Nafasi ya Mwenyekiti
haikuwa na mgombea wakati Mawazo Maso aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi
ya Makamu Mwenyekiti alipata kura nyingi za hapana. Nafasi zilizo wazi
zitajazwa katika uchaguzi mdogo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment