Nafasi Ya Matangazo

September 26, 2012

 
Taasisi ya Mawasiliano ya Afrika Mashariki (EACO) imefungua ofisi za sekretarieti yake mjini Kigali, Rwanda ili kuratibu na kurahisisha utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Taasisi hiyo iliichagua Rwanda kuwa makao yake makuu ya kudumu karibu miezi 14 iliyopita katika mkutano wake wa 18 uliofanyika mjini Kigali, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki linaripoti.
Kufuatia uamuzi huo, ofisi hiyo iliyofunguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na kuanza rasmi kazi zake ni inahusisha wajumbe wa bodi ya wakurugenzi tu.
EACO ni taasisi ya kikanda inayoshughulika na udhibiti wa masuala ya posta, mawasiliano na utangazaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Sekretarieti hiyo itafanyakazi zake katika makao yake makuu ya muda yaliyomo ndani ya ofisi za Taifa za Mamlaka ya Mawasilino nchini Rwanda zilizopo katikati ya jiji la Kigali.
Lakini mipango ipo mbioni ya kujenga ofisi zake za kudumu kwa ajili ya masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ya taasisi hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Waziri wa Masuala ya EAC wa Rwanda, Monique Mukaruliza alielezea uzinduzi huo kuwa ni hatua moja kubwa katika mwenendo mzima wa kuleta mtangamano wa jumuiya hiyo.
‘’Kila wakati tunapofanya vikao vya Baraza la Mawaziri huangalia itifaki tulizotia saini, maamuzi tuliyotoa na hujiuliza sisi wenyewe ni maendeleo gani tumeyafikia. Tuna uhakika kwamba wananchi wa Afrika Mashariki wameanza kunufaika na mtangamano tunaouzungumzia? Huu ni mfano hai kwamba wanaafrika Mashariki wanaweza kujipanga wenyewe na kufanya jambo la maana,’’ alisema.
Waziri Mkaruliza ameahidi kutoa ushirikiano unaohitajika kwa EACO ili kufanikisha malengo yake.
‘’Ndoto yetu katika mtangamano ili kupata umoja, maendeleo na ushirikiano sasa inaendelea kuwa ya kweli kupitia uzinduzi wa ofisi za sekretarieti ya EACO,’’ alisema Salvatory Nizigiyimana, Mwenyekiti wa EACO.
Nizigiyimana ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Burundi (ARCT) alielezea matumaini yake kuwa taasisi hiyo itakuwa chachu ya kuleta maendelea kwa kukuza mawasiliano katika kanda hiyo.
Posted by MROKI On Wednesday, September 26, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo