Nafasi Ya Matangazo

April 19, 2012

25 TWIGA STARS KAMBINI APRILI 20
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa ameita wachezaji 25 watakaoingia kambini kesho (Aprili 20 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe inayotarajiwa kuchezwa Aprili 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 
Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Twiga Stars kabla ya mechi ya mashindano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia itakayochezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa kabla ya timu hizo kurudiana jijini Dar es Salaam wiki mbili baadaye.
 
Baada ya kuripoti kambini jioni, wachezaji hao watafanyiwa vipimo vya afya (medical examination) siku inayofuata (Aprili 21 mwaka huu) na kuanza mazoezi Aprili 22 mwaka huu. Kambi ya timu hizo itakuwa kwenye hosteli za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani.
 
Wachezaji walioitwa ni Amina Ally kutoka Sekondari ya Lord Baden, Asha Rashid, Aziza Mwadini (New Generation, Zanzibar), Etoe Mlenzi (JKT Mbweni), Evelyne Sekikuto (Mburahati Queens), Fadhila Hamad (Uzuri Queens), Fatuma Bashiri (Simba Queens), Fatuma Khatib (Mburahati Queens) na Fatuma Mustafa (Sayari).
 
Wengine ni Fatuma Omari (Sayari), Hanifa Idd (Uzuri Queens), Maimuna Said (JKT Mbweni), Mariam Aziz (Tanzanite), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens), Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens), Mwapewa Mtumwa (Sayari) na Rehema Abdul (Lord Baden).
 
Kikosi hicho pia kina akina Rukia Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Siajabu Hassan (Evergreen), Sophia Mwasikili (Luleburgaz Spor Kulubu, Uturuki), Veneranda Mtamo (Tanzanite), Zena Khamis (Mburahati Queens) na Zena Said (Uzuri Queens).
 
 
KUONA NGORONGORO HEROES, SUDAN 3,000/-
Kiingilio cha chini cha mechi ya kuwania kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Sudan itakayochezwa Jumamosi (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 3,000.
 
Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni, na viingilio vingine vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati VIP itakuwa ni sh. 15,000.
 
Sudan inatarajia kuwasili leo mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 30 na itafikia hoteli ya Rungwe iliyoko maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam. Jioni itafanya mazoezi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
 
Ngorongoro Heroes tayari iko kambini chini ya Kocha Kim Poulsen, na leo inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Sudan yenyewe itafanya mazoezi kwenye uwanja huo kesho.
 
Kesho (Aprili 20 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutakuwa na mkutano kati ya makocha wa timu zote mbili na Waandishi wa Habari.
 
MKUTANO MKUU TFF APRILI 21, 22
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utafanyika kwa siku mbili (Aprili 21 na 22 mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam.
 
Wajumbe wa mkutano huo watawasili jijini kesho (Aprili 20 mwaka huu) na watafikia kwenye hoteli ya Royal Valentino. Wajumbe wanatoka katika vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.
 
Mkutano huo utakaoanza saa 3 asubuhi utakuwa na ajenda kumi na moja. Baadhi ya ajenda hizo ni hotuba ya Rais wa TFF, taarifa ya utendaji ya mwaka 2011, bajeti ya mwaka 2012 na taarifa ya ukaguzi wa hesabu (audited accounts).
 
JKT RUVU, SIMBA ZAINGIZA MIL 30/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya JKT Ruvu na Simba lililochezwa jana (Aprili 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 30,095,000.
 
Jumla ya watazamaji 8,362 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000. Watazamaji 7,310 kati ya hao walishuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000.
 
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,590,762.71 kila klabu ilipata sh. 4,455,551.19, uwanja sh. 1,485,183.73.
 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 1,485,183.73, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 297,036.75 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 297,036.75.
 
Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 742,591.86, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 148,518.37 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 1,485,183.73.
 
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000 na nauli ya ndani kwa mtathmini wa waamuzi sh. 10,000.
 
Mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna, mtathmini wa waamuzi na waamuzi sh. 120,000, gharama ya tiketi sh. 3,750,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
 
Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 585,340 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 510,720.
 
SIMBA, MORO UNITED KUCHEZA USIKU
Mechi ya Ligi ya Vodacom kati ya Simba na Moro United iliyokuwa ichezwe Aprili 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imerudishwa nyuma hadi Jumatatu ya Aprili 23 mwaka huu kwenye uwanja huo huo na itaanza saa 1 kamili usiku.
 
Mabadiliko hayo yamefanyika ili kuipa Simba fursa ya kujiandaa vizuri kwa mechi yao ya Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Aprili 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
 
Pia mechi kati ya Azam na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Aprili 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam imesogezwa mbele hadi Aprili 22 mwaka huu kupisha mechi ya U20 kati ya Tanzania na Sudan itakayochezwa Aprili 21 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Mechi nyingine mbili zimefanyiwa marekebisho; Coastal Union na Kagera Sugar zilizokuwa zicheze jijini Tanga, Aprili 29 mwaka huu, mechi yao imesogezwa hadi Aprili 30 mwaka huu ili kupisha shughuli za Mei Mosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Nazo Azam na Toto Africans zilizokuwa zicheze Aprili 26 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, sasa zitacheza Aprili 28 mwaka huu.
Posted by MROKI On Thursday, April 19, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo