NI BAADA YA JOPO LA MADAKTARI MUHIMBILI KUMFANYIA UCHUNGUZI
MSANII nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba amefariki dunia kutokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo linalojulikana kitalaamu kama Brain Concussion, taarifa za kitabibu zimeeleza.
Taarifa hizo za ndani, zilizopatikana jana baada ya jopo la madaktari bingwa watano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo, zimeeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa. Mmoja wa madaktari hao ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema waligundua tatizo hilo baada ya kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.
“Tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:45 mchana na tukagundua kuwa marehemu alifariki kutokana na mtikisiko wa ubongo kwa kitaalamu, Brain Concussion,” alisema daktari huyo. Alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo ambao husababisha kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure) “Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu ya nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka” alisema daktari huyo na kuongeza kuwa mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wake.
“Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndiyo maana tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo ndizo dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji.”
“Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo huweza kutokwa na mapovu mdomoni na hukoroma kabla ya kukata roho na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki.”
Daktari mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo ambaye pia aliomba jina lake lisitajwe alisema ubongo wa mwigizaji huyo ulikuwa umevimba na kushuka karibu na uti wa mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji. Alisema sehemu ya maini na majimaji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine katika mwili huo.HABARI ZAID BOFYA HAPA.
0 comments:
Post a Comment