MAREKEBISHO YA RATIBA LIGI KUU YA VODACOM
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho madogo kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kutumika kwa sherehe za kitaifa za kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mechi namba 111 kati ya Toto Africans na African Lyon ambayo kwa mujibu wa ratiba ilikuwa ichezwe Februari 5 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza sasa itachezwa Aprili 18 mwaka huu.
Mabadiliko hayo yamefanyika baada ya wamiliki wa Uwanja wa CCM Kirumba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kueleza kuwa watautumia kwa sherehe za kuzaliwa chama chao, hivyo hautakuwa na nafasi kwa Februari 4, 5 na 6 mwaka huu.
Uamuzi huo umesababisha pia mabadiliko kwa mechi nyingine mbili. Mechi namba 168 kati ya Villa Squad na African Lyon iliyokuwa ichezwe Aprili 18 mwaka huu Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, sasa itachezwa Aprili 22 mwaka huu.
Pia mechi namba 170 kati ya Azam na Toto Africans iliyokuwa ichezwe Aprili 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam sasa imerudishwa nyuma hadi Aprili 26 mwaka huu ambayo ni Sikukuu ya Muungano.
VIINGILIO MECHI YA TWIGA STARS, NAMIBIA
Kiingilio cha chini kwa mechi ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia itakayochezwa Jumapili (Januari 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa sh. 2,000.
Kiwango hicho ni kwa washabiki kwa viti vya bluu na kijani. Viti hivyo kwa pamoja vinachukua jumla ya watazamaji 36,693 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua washabiki 60,000.
Pia kutakuwa na kiingilio cha watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 ambacho ni sh. 1,000. Watoto watakaotumia tiketi hizo wanatakiwa kuingia uwanjani wakiwa na wazazi au walezi wao.
Viingilio vingine kwa mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 5,000 kwa VIP B na C n ash. 10,000 kwa VIP A.
Namibia inatarajia kuwasili nchini Ijumaa (Januari 27 mwaka huu) saa 12.45 jioni kwa ndege ya South Africa Airways.
LIGI KUU VODACOM KUWANIA UBINGWA WA BARA
Mzunguko wa 14 wa Ligi Kuu ya Vodacom unamalizika kesho (Januari 25 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa kwenye viwanja tofauti jijini Dar es Salaam.
Simba itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Viingilio vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP B na C, sh. 15,000 kwa VIP A.
Nayo Azam itakuwa mgeni wa African Lyon katika mechi namba 97 itakayochezwa Uwanja wa Chamazi. Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 10,000 kwa Jukwaa Kuu na sh. 3,000 mzunguko.
YANGA YATAKIWA KUMLIPA NJOROGE SH. MILIONI 17
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kupitia kitengo chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute Resolution Chamber- DRC) limeagiza klabu ya Yanga kumlipa mchezaji John Njoroge sh. 17,159,800 ikiwa ni fidia kwa kuvunja mkataba wake kinyume cha taratibu.
Uamuzi huo wa DRC chini ya Jaji Theo van Seggelen ambaye ni raia wa Uholanzi ulifanywa Desemba 7 mwaka jana jijini Zurich, Uswisi na kutumwa TFF kwa njia ya DHL, Januari 17 mwaka huu.
Njoroge ambaye ni raia wa Kenya aliwasilisha kesi yake FIFA kupinga Yanga kuvunja mkataba alioingia wa kuichezea timu yao kinyume na makubaliano. Mchezaji huyo hivi sasa anachezea timu ya Tusker ambayo ni mabingwa wa Kenya.
Yanga ina siku nne za kukata rufani kupinga uamuzi huo kuanzia tarehe iliyoupokea kama inataka kufanya hivyo. Klabu hiyo inatakiwa iwe imeshamlipa Njoroge ndani ya siku 30 tangu ilipopokea uamuzi huo. Ikishindwa kulipa ndani ya muda huo, itatozwa riba ya asilimia 5 kwa mwaka ya fedha hizo.
Ikiwa Yanga itashindwa kulipa ndani ya muda huo vilevile suala hilo litafikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA kwa hatua zaidi.
0 comments:
Post a Comment