Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia kuondoka kesho (Novemba 9 mwaka huu) saa 9 alasiri kwa ndege ya Kenya Airways kwenda N’Djamena kwa ajili ya mechi ya kwanza ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa Novemba 11 mwaka huu.
Msafara wa Stars wenye watu 40 ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella utawasili N’Djamena kesho hiyo hiyo saa 1.15 usiku kwa saa za huko ambapo kwa hapa nyumbani ni saa 3.15 usiku.
Wachezaji katika msafara huo watakuwa wote 21 walioko kambini, watu sita kutoka Benchi la Ufundi wakiongozwa na Kocha Jan Poulsen, wajumbe wawili wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na washabiki.
Stars ambayo iliagwa jana saa 1 usiku kwa kukabidhiwa bendera na Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi itarejea nchini Novemba 13 mwaka huu saa 7.25 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines na kwenda moja kwa moja kambini New Africa Hotel kujiandaa kwa mechi ya marudiano itakayochezwa Novemba 15 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment