Nafasi Ya Matangazo

October 16, 2011

VITENDO vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) vimeibuka tena wilayani Geita mkoani Mwanza, baada ya mlemavu mmoja wa ngozi kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kulia pamoja na kukatwa mkono wa kushoto.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Nyaruguguna, Kata na Tarafa ya Nyang’hwale ambapo mlemavu huyo, Adam Robert (14), mwanafunzi wa darasa la nne, alivamiwa na kukatwa mkono wa kulia na kisha kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kushoto.

Akisimulia mkasa huo, mlemavu huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita akiuguza majeraha yake, alisema alikumbwa na mkasa huo saa 1:40 usiku akiwa nyumbani kwao ambapo alivamiwa na mtu mmoja waliyekuwa wanakula naye chakula nje ya nyumba.

Akizungumza kwa shida katika kitanda namba 5 alikolazwa, alisema siku ya tukio saa 12 alifika nyumbani kwao mtu huyo akidai amekwenda kuangalia ng’ombe wake waliokuwa wamepotea ambapo walianza maongezi na yeye juu ya upotevu wa ng’ombe hao.

‘‘Wakati tuko nje na baba, mtu huyo alifika na kubisha hodi kisha tukamkaribisha tukampa kiti akakaa ndipo akaanza kutueleza kuwa anawatafuta ng’ombe wake waliopotea machungani.

Tukaendelea kuzungumza naye hadi tulipoletewa chakula hapo nje tukaanza kula,’’ alisema na kuongeza: ‘‘Ghafla mvua ikaanza kunyesha ikabidi tuhamie ndani, baba akawa amechukua ugali akatangulia ndani mimi nikabeba mboga yule mtu akabeba kiti chake, wakati tunaingia ndani nilikuwa katikati ya baba na mtu huyo, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida kabla sijaingia ndani yule mtu akanishika na kunivuta nje”.

Alisema baada ya kuvutwa mtu huyo alianza kumkata mkono wake wa kushoto upande wa begani wakati huo akiwa amelala chini akijitupatupa na baada ya kuona ameshindwa kuukata na kuunyofoa mkono kuanzia kwenye kiganja, akaacha na kuanza kuukatia tena kwenye kiwiko.

“Aliposhindwa pia kuukatia kwenye kiwiko aliamua kuugeukia mkono wangu wa kulia na kukata vidole vyangu vitatu vya mkono huo na kuvinyofoa kabisa, wakati huo baba alishindwa afanye nini akabaki kukimbilia huku na kule na wakati huo kaka yangu alikuwa amejificha kwenye nyumba nyingine na kilichonishangaza sana ni kwamba pamoja na kupiga sana kelele za kuomba msaada hakuna mtu hata mmoja aliyejitokeza kwa ajili ya kuja kunisaidia,” aliongeza kusema.

Akizungumzia tukio hilo baba mzazi wa mlemavu huyo, Robert Tangawizi (36) alisema wakati tukio hilo linatendeka alikuwa kama vile amechanganyikiwa na kushindwa kabisa kumuokoa mwanawe muda wote wa purukushani kati yake na mhalifu huyo na kwamba alishikwa na bumbuwazi na hasa baada ya kumuona mtu ambaye walikuwa wanakula naye chakula kwenye meza moja amegeuka mhalifu kwa mwanawe.

“Yaani kweli mimi sijui hata kwa kweli nashindwa hata kuelezea tukio hili, kwa sababu nashangaa kwamba mtu ambaye tumemkaribisha vizuri na kumpatia kiti kwa heshima zote na tukaanza kula naye chakula ghafla anageuka na kuwa muuaji na kufanya kitendo cha kikatili kama hiki nilishindwa kabisa nifanye nini, kwa sababu kwa muda wote sikuamini kama kweli ni mtu huyu huyu ndiye alikuwa akifanya jambo hili,’’ alisema baba mzazi wa mlemavu huyo.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dk. Omar Dihenga amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo, na kufafanua kwamba majeraha aliyoyapata majeruhi huyo ni makubwa lakini madaktari wa hospitali hiyo wamefanya kila linalowezekana katika kuhakikisha kuwa wanampatia matibabu ya uhakika.

“Wamemkata vibaya sana huyu mtoto lakini madaktari wamejitahidi sana kwa bahati nzuri ushonaji wa maeneo yaliyojeruhiwa umekwenda vizuri isipokuwa ni vidole vyake vitatu ambavyo vimenyofolewa kabisa, hata kama tungevipata isingewezekana kuviunganisha kwa sababu kwa namna ambavyo vimekatwa ni vigumu kuvirejesha katika hali yake ya kawaida, kwa hiyo huu tayari ni ulemavu wa kudumu,’’ alifafanua Dk. Dihenga.

Polisi wilayani hapa wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba bado wanaendelea na mahojiano na majeruhi, wazazi na majirani ili kujua namna ambavyo wanaweza kuwanasa wahusika wa tukio hilo.

Vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaani maalbino hayajatokea katika Wilaya ya Geita katika kipindi cha kuanzia Januari mwaka 2009 hadi tukio la juzi ambalo linaonekana kuamsha hofu kwa mara nyingine kwa watu wenye ulemavu huo wilayani hapa ambao idadi yao ni 93.

Kwa nchi nzima, mauaji hayo na ukatili huo unaofanyika zaidi katika Kanda ya Ziwa, zaidi ya watu 50 wameathirika, ama kwa kukatwa viungo vyao au kwa kuuawa kati ya mwaka 2007 na mwaka jana, lakini nguvu kubwa ya kupingana na mauaji hayo ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilirudisha nyuma matukio ya unyanyasaji dhidi ya maalbino.

Katika kipindi hicho, watu kadhaa walikamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola, huku watatu kati ya watano waliokamatwa miaka mitatu iliyopita wakituhumiwa kumuua mtoto (albino), Esther Charles wakihukumiwa kunyongwa hadi kufa Juni 3, mwaka huu, baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora.

Jaji Laurence Kaduri aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, aliwahukumu kunyongwa hadi kufa washitakiwa hao, Charles Kalamuyi (zungu), Masumbuko Madada (Sumbu) na Merdadi
Maziku (Machunda) kutokana na kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila shaka yoyote.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa takribani saa nne, mshitakiwa mwingine Peter Mahina, aliachiwa huru baada ya kukosekana ushahidi wa kumuunganisha wakati mshitakiwa wa tano Malalija Jiduta, alifariki dunia akiwa rumande wakati kesi hiyo haijaanza kusikilizwa.

Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na jopo la mawakili watatu Neema Ringo, Prudence Rweyongeza na Janeth Sekule, uliiambia Mahakama kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Oktoba 19, 2008 huko katika kijiji cha Shilela Usala, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, washitakiwa walimuua mtoto huyo kwa kumkata mapanga sehemu za mabega, wakikinga  damu yake na kutokomea huku wakimwacha mlemavu huyo akiwa hajitambui na baadaye akapoteza maisha kutokana na kuvuja damu nyingi.

Hivi karibuni akiwa katika ziara yake mkoani Mara, Pinda alieleza kuridhishwa na kupungua kwa matukio ya mauaji na ukatili dhidi ya albino akisema ukatili huo ni wa hali ya juu, unaosikitisha na kuhuzunisha na aliwaomba Watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili aepushe kutokea kwa mauaji mengine ya aina hiyo.
Chanzo:Habarileo.
Posted by MROKI On Sunday, October 16, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo