Nafasi Ya Matangazo

August 08, 2011

Tofauti za dini zisiwe chanzo cha mifarakano

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kutoruhusu imani za dini ama tofauti za imani miongoni mwa madhehebu mbali mbali ya dini kuwa chanzo cha mifarakano ndani ya jamii.

Mheshimiwa Kikwete pia amewataka viongozi wa dini kusaidia kujenga tabia ya uvumilivu na  kuheshimiana miongoni mwa viongozi na waumini wa dini na madhehebu mbali mbali ya dini nchini kama msingi mkuu wa imani ya Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amewataka viongozi hao kuepukana na mwenendo wa kukashifu dini za watu wengine ama madhebebu ya waumini wengine akisisitiza kuwa hata wao viongozi wa dini hawawezi kutoa huduma zao za kiroho katika hali ya mifarakano na kutoelewana.

Rais Kikwete amewaomba viongozi wa dini kuombea amani na utulivu nchini ili kuwajengea wananchi mazingira mwafaka ya kujiletea maendeleo ya haraka zaidi. Rais Kikwete aliyasema hayo jioni ya jana, Jumapili, Agosti 7, 2011, wakati alipozungumza kwa ufupi baada ya kuwa amefuturu na viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali ya dini kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Ikulu, Dar Es Salaam.

Rais Kikwete aliwaambia viongozi hao: “Nyie mko karibu na Mwenyeji Mungu kuliko sisi waumini wa kawaida. Nawaomba mtusaidie kuombea nchi yetu ili tuendelee kuwa na amani na utulivu. Tuombee tupate mvua za heri. Tuombee tupate mavuno ya uhakika. Tuombee mabwawa yetu yajae. Tupate umeme wa uhakika.”

Ameongeza Mheshimiwa Rais: “ Nawaombeni nyie viongozi wa dini kusaidia kuleta utulivu na maelewano kwa sababu hatutanufaika katika hali na mazingira ya uhasama.

Haijawahi kutokea mahali popote duniani watu wakanufaika katika mazingira ya uhasama, na uhasama wenyewe unapotokana na tofauti za dini unakuwa hatari zaidi.”

Amesisitiza: “ Ni wajibu tuheshimu dini na madhehebu ya dini za wenzetu. Ni lazima tuvuliane kwa tofauti zetu. Sisi wenyewe katika Uislamu tunayo matawi mbali mbali. Ni lazima tuvumiliane katika tofauti zetu kwa sababu tofauti zipo na zitaendelea kuwepo. Na tofauti zenyewe hazitamalizwa na migongono ama kukashifiana. Tukiepuka kukashifiana tutaishi kwa raha mustarehe pamoja na kwamba tutabakia na tofauti zetu.”

Viongozi hao wa dini wamekuwa kundi la pili la wanajamii kualikwa Ikulu na Rais Kikwete kwa ajili ya kula nao futari wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan mwaka huu.

Kundi la kwanza kualikwa na Mheshimiwa Rais lilikuwa la watoto yatima ambalo lilifuturu na heshimiwa Rais na Mama Salma Kikwete Ijumaa iliyopita, Agosti 5, 2011.
Imetolewa na: 
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
 Ikulu, DAR ES SALAAM.
 08 Agosti, 2011
Posted by MROKI On Monday, August 08, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo