Nafasi Ya Matangazo

August 09, 2011

Diwani wa Kata ya Hai Mjini Mkoani Kilimanjaro Ombaeli Lema (37) na Mkewe Rachel Uronu (35) wamefariki Dunia Kwenye Ajali Ya Gari.

Ajali  hiyo iliyotokea katika barabara kuu ya Sanya Juu, Bomang’ombe katika  maeneo ya Kwa Mose kijiji cha Mungushi ilihusisha magari mawili aina ya  Fuso na Toyota Pick up yaliyogongana uso kwa uso.

Kwa  mujibu wa taarifa kutoka kwa kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro,  Absalomu Mwakyoma ajali hiyo ilitokea Agosti saba mwaka huu, majira ya  saa tatu usiku katika kijiji cha Mungushi Wilayani Hai Mkoani  Kilimanjaro.

Alisema  katika ajali hiyo lori la mizigo aina ya Fuso lenye namba T 279 ACL  lilikuwa likiendeshwa na Hezekieli Mwafifi liligongana na gari dogo aina  ya Toyota Pick Up lenye namba za usajili T954 AFU lililokuwa  likiendeshwa na marehemu Ombaeli Lema.

Alisema  gari hilo dogo, lililokuwa na Diwani pamoja na mkewe waliokuwa wametoka  nyumbani kwa wazazi wao katika kijiji cha Ivaeny maeneo ya Kibong’oto  na walikuwa wakirejea nyumbani kwao maeneo ya Bomang’ombe Wilayani Hai.

Alisema  gari aina Fuso lililokuwa likielekea Sanya Juu lilipofika eneo la tukio  ndipo lilipogongana na gari hilo dogo na kusababisha vifo vya  wanafamilia hao.

Kwa  mujibu wa taarifa toka kwa Kamanda alisema Ombaeli Lema alifia papo  hapo na mkewe alifariki mara baada ya kufikishwa katika hospitali ya  Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi.

Hata  hivyo kamanda huyo alisema kuwa dereva wa lori anashikiliwa na Jeshi na  polisi huku upelelezi zaidi ukiendelea na mwili wa marehemu Ombaeli  Lema umehifadhiwa katika hospitali Kibong’oto huku mwili wa mkewe Rachel  umehifadhiwa katika hospitali ya KCMC.

Posted by MROKI On Tuesday, August 09, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo