Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Angetile Osiah, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Kili Taifa Cup 2011. Kulia ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe.
Mashindano ya Kili Taifa Cup 2011 yamezinduliwa jijini Dar es Salaam leo.
Uzinduzi huo uliokuwa na kila aina ya nderemo na vifijo ulivutia wadau mbalimbali wa soka na wale wanaotoka katika tasnia ya habari, na kufanyika katika Safari Pub, ndani ya viwanja vya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Kilimanjaro Premium Larger kudhamini mashindano ya Kili Taifa Cup lakini ni mara ya tano kwa TBL kufadhili mashindano hayo, ambapo kabla bidhaa iliyotumika kufadhili ilikuwa Safari Lager. Align Center
Mashindano ya mwaka huu yanayokwenda na dhima ‘Fikisha Soka la Tanzania Katika Kilele Cha Mafanikio’ yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 7 katika hatua ya mtoano na yatafanyika kwenye vituo sita vilivyoteuliwa.
Vituo vilivyoteuliwa mwaka huu ni pamoja na Mwanza, Moshi, Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya na Lindi. Jumla ya timu 24 kutoka mikoa mbalimbali zitashiriki kwenye mashindano hayo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Oseah aliipongeza Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwa mstari wa mbele kukuza kandanda nchini.
Alisema kwamba mashindano ya Kili Taifa Cup yamekuwa chanzo kikubwa zaidi cha kufuatilia na kupata vipaji kutoka ngazi za chini mikoani na kwamba mashindano yamekuwa yakikua mwaka hadi mwaka, akitoa mfano wa fainali za mwaka jana zilizoshuhudia timu mbili kutoka mikoani, Singida na Lindi zikipigania zawadi ya kwanza, ambapo Singida iliibuka bingwa.
“Tumekuwa tukishuhudia katika nyakati zilizopita timu za Dar es Salaam tu lakini mwaka jana ilikuwa tofauti tuliposhuhudia timu kutoka mikoani zikicheza fainali,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, David Minja alirejea lengo la kampuni yake, kupitia Kilimanjaro Premium Lager kudhamini mashindano hayo, akisema kwamba ni moja ya matukio makubwa zaidi ya soka nchini yanayozalisha wachezaji kwa ajili ya klabu mbalimbali kubwa nchini na timu ya taifa.
Alisema kwamba kampuni yake imetoa zaidi ya Sh milioni 800 kwa ajili ya mashindano hayo yatakayodumu hadi mwishoni mwa mei. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya maandalizi ya timu, usafiri, malazi na vifaa vya michezo.
“Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na TFF kuhakikisha kwamba mashindano haya yanafanikiwa na tunaamini kwamba haya ya mwaka huu yatakuwa na mvuto zaidi. Tunawaalika mashabiki kujitokeza kwa wingi kushangilia timu zao,” alisema.
Zawadi za mwaka huu, akaongeza Minja, zimeboreshwa zaidi ikilinganishwa na mwaka jana, ambapo mshindi wa kwanza ataibuka na Sh milioni 40.
Mshindi wa pili atapata Sh milioni 20 wakati yule wa tatu atazawadiwa Sh milioni 10.
Zawadi nyingine ni pamoja na Sh milioni 2 kwa golikipa bora, Sh milioni 2.5 kwa mfungaji bora, Sh milioni 2 kwa kocha bora, Sh milioni 2 kwa refarii bora na Sh milioni 2 imetengwa kama zawadi kwa uchezaji wenye nidhamu. Baada ya kila mchezo, mchezaji bora atatangazwa na kuzawadiwa Sh 100,000.
“TBL imekuwa ikijihusisha na soka kwa muda mrefu na imedhamiria kuendelea katika hili na udhamini kwenye soka,” alisema Minja.
0 comments:
Post a Comment