Nafasi Ya Matangazo

April 08, 2009

Busara za Mfuga Ndevu

Na Father Kidevu
JAMANI parapanda, Parapanda italia parapandaaa, walio DECI watakuja kujutia fedha zao x2 Nayo serikali itakosa wapigakura 2010 x2, huu ni wimbo ambao hivi sasa unaibwa na serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wakala wa Soko la fedha na Mitaji (CMSA) kwa watanzania wapatao laki saba ambao ni wanachama wa Kapuni ya DECI (T) Limited ya jijini Dar es Salaam.

Mashairi ya mapambio hayo ambayo mmoja akiimba Ubeti na mwingine anaitikia kiitikio unafurahisha sana katika masikio yangu na bila shaka hata katika masikio yako. Lakini leo hiki kiitikio ndio kinanipa shida hasa nikisoma alama za nyakati na kupata hofu kuwa siku za vilio na wasaga meno yaja.

Takriban wiki mbili sasa tumeanza kusikia BoT na CMSA wakisema kuwa DECI si kampuni halali ya kuendesha biashara ya fedha nchini kwani haina baraka (vibali) vya taasisi hizo nchini. Na kwa mujibu wa sheria za nchi hii ni kosa la jinai kuendesha biashara ya Upatu.

Mimi nashangaa kumsikia huyu jinai akisema kuwa DECI siyo halali ana kisheria atamfungia na akifungiwa basi watanzania laki saba watapoteza bilioni zao walizoziweka kwa mtumishi huyio wa Mungu badala ya kuziweka Benki ambako wamegundua kuwa kuna wadudu waharibifu walao mbegu bora.

Hahahah na wewe unashangaa nini kwani hujui sera ya DECI ni ‘Vuna kadri ulivyo opanda mbegu’ hivyo ndomaana watu wengi ‘tukaenda’ kupanda mbegu huko ya fedha na tukaanza kuvuna mapesa na kufanya maisha bora aliyosema Rais Jakaya Kikwete kuwa kweli ilhali zamani tuliona ni ndoto.

Mwanzoni wakati inaanza watu wakazani ni masihara haiwezekani upande fedha sh 20,000 ambao ndio mshahara wa juu wa wafanyakazi wa ndani na wahudumu wa bar hapa nchini halafu uvune sh 40,000 ndani ya miezi 3 ilhali fedha kama hiyo ukiipanda huko ambako BoT imetoa vilali ndani ya hiyo miezi mitatu unaweza kukuta salio ni sh 5,000 sawa na pumba.

Sasa ‘why are we poor’ kwanini sisi ni masikini ilhali kuna mashamba yaliyo na rutuba ya kutosha kupanda mbegu na ukavuna bila tatizo, leo eti shamba hilo tunaambiwa ni feki na halitufai tuachane nalo. JK umewasikia hawa BoT lakini? Wanakutakia mema kweli kwa hawa wapigakura wako.

Huenda Gavana wa BoT angekuwa ni mpigiwa kura kama wewe JK walahi asingethubutu kusema DECI haifai na badala yake angetafuta mbinu za kuwasaidia wapigakura kuzinusuru mbegu zao pindu ukame utakapotokea huko shambani kwa kuwatafutia zana za umwagiliaji kwa maana ya DECi kufungua zamana BoT.

Kidevu la msinione mbaya kwa kukuna ndevu zangu zilizo jaa chawa wa umasikini maan asikuwahi jua kama kuna DECI maana visenti vyangu ninavyopata huku nanihii ningevipanda huko sasa ningekuwa sihangaiki kodi ya nyumba.

Unajua nashangaa inakuaje hawa jamaa wanaosemwa kuwa ni ‘matapeli’ wanatozwa kodi? Kha! Kumbe wewe ulikuwa hujui kuwa DECI ni walipa kodi wazuri sana hapa nchini na TRA wanawatambua kupitia namba hii TIN NO 105-797-095.

Takwimu zinaonyesha kuwa DECI inamatawi zaidi ya 17 Tanzania na imesha fanya mambo makubwa kwa wanachama wake ambao hawachagui dini,utaifa,rangi na hata afya ya mwanachama maana naambiwa kuwa zaidi ya Albino 130 wananufaika na DECI na moja wa wakurugenzi wa DECI mkoani Tanga ni Albino na amepewa gari ya kutembelea ya zaidi ya milioni 40.

Nikikumbuka wimbo wangu hapo juu wa Parapanda na nyakati hizi tunazokwenda za Uchaguzi wa serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2010 patakuwa hapatoshi. Hapatatosha kwa maana kuwa hawa wapigakura laki 7 ambao ni wanachama wa DECI wakigoma kupiga kura au kuto kipigia chama tawala ambacho watendaji wake wanaokitumikia wanataka kulitia magugu maji shamba lao itakuaje.

Wapiga kura lakini saba ni sawa na majimbo 21 ya Uchaguzi huko vijijini kwetu ambako wapigakura wanahitajika kutawaza Mbunge hawazidi 35,000, hili nalithibitisha na uchaguzi uliomtia madarakani Mbunge wa Mbeya Vijijini Mchungaji Lackson Mwanjali alishinda kiti hicho kwa kura 32,887.

Hebu nimabie kwa mpango huu hao watu laki saba tu watawanyima kura wabunge 21 kwa kosa dogo ambalo linahitaji ushauru tu kunusuru DECI kufungwa. Lakini pia tujue hao laki saba ni mmoja kati ya wanafamilia 4 ambao walikuwa wananufaika na DECI kutokana na eidha baba au mama alipanda mbegu ya fedha DECI.

Zidisha 700,000 mara 4 ni sawa na wapigakura milioni 2,800,000 ambao watasema NO kwako wewe uliye madarakani na chama chako kimeshindwa kututetea ili DECI isifungwe, hiyo ndo Parapanda itakapolia lazima watu watasaga meno.

Msije kusema Kidevu mchochezi, Wabunge sheria zetu za nchi nafikiri sio Msaafu wala Biblia ambavyo hatupaswi kuvibadili, lakini sheria ngapi tulibadili hadi sheria hii inayoibana DECI ishindikane?. Hakuna naimani inawezekana.

Si juzi tu tulifanikiwa kubadili sheria ya Pikipiki na Bajaji kuweza kubeba abiria kama daladala na Taxi hapa mjini kwakuwa asilimia kubwa ya wateja wake ni walalahoi? Sasa hili la DECI kuishauri iwe na dhamana ya wateja wake tunashindwa nini hadi tukazanie kuipiga pingu.

Ama tulifanya hivyo kwa bajaji na pikipiki kwa sababu mheshimiwa nanihii una Bajaji zako pale njiapanda ya Kawe na zile bodaboda za Best yako kule bush, hahahahha unacheka nini sasa, pigia mstari DECI isife.

‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania…kwa Tanzania yenye neema inawezekana’…Rais Kikwete ulikuwa na nia nzuri sana na nchi yetu lakini hawa vijana wako wapiga makofi pindi unapohutubia ndo wanatufanya tukate tama ya maisha na tujiandae tukipata nauri tuje kukusalimia Mjomba.

Neema aliyoizungumza Mjomba JK hapa si hayo madini ambayo sisi wenye jembe la mkono hatuwezi kuchimba Tanzanite na Almasi hadi mje wenye makatapila, hapoana ni hata busara za kufikiria njia ya kusaidiana kukwamuana kiuchumi kama huyu Mtumishi wa Mungu aliyeamua kubuni DECI kwaajili ya waumini wake na baadae kuona ina faa kukaribisha wengine na hadi kuwa ilivyo sasa.

Mimi naimani kuwa Serikali inaweza kuwasaidia hawa Wapiga kura ambao wengine nasikia wanasomesha watoto vyuo vikuu na hata kujenga majumba kutokana na pesa za DECI kuweza kuishauri Taaisi hiyo kuchota fedha kiasi kwaajili ya Dhamana na tayari walishaomba kujisajili hivyo lakini BoT wakesita kwakuwa Polisi ilikuwa wanachunguza.

Kila kada ya mtanzania inanufaika DECI hata wakurugenzi nao wamo, na wameamua kwenda kucheza kamari baada ya kuona zile fedha za Mjomba JK alizotoa kuwainua walala hoi zimeliwa na walala ubwete, walao ugali na mboga saba na si ugali wa dona na mboga moja chukuchuku.

Lakini Mh! Kwanini BoT walie sana na hili la DECI kuwa haliwatambui ilhali kuna hivi vyama vya kuweka na kukopa maarufu katika maofisi na mijini SACCOS, Saccos nasikia kuwa haitambuliwi BoT lakini inatoa mkopo hadi milioni 100 na huwezi kupata mkopo kama hujaweka mbegu yako ya kutosha.

Ukisha vuna hizi za Saccos unatakiwa utoe ‘ngoto’ yaaani kilemba kwa mavuno yako. (kule kijijini kwetu ilikuwa mtu akikodisha shamba akalima akivuna kama alipata mahindi au mtama gunia mbili basi atapeleka debe mbili kwa mwenye shamba). Kama una shamba kubwa ukawagawia watu wewe wala hulimi mwaka mzima unakula vya watu t undo BENKI zetu.

Hela zetu tunaweka Benki lakini pindi ukitaka kuchukua zaidi ufanikishe mambo yako ‘fasta’ watachekelea na kukupa ila ukivuna ulete na riba ‘kibwena’. Swali langu ni kwa BoT hizi Saccos mnazitambua?. Na umakini wenu huu inakuaje mkumbuke shuka wakati kuna kucha au mnanjama maana nyie mmesha vuna sasa mnafungulia kuku wachakure mashimo wale mbegu za wenzenu walizopanda shamani kwao DECI.

Tunamwomba mheshimiwa rais awachukulie hatua za haraka wahusika wote ambao husimamia taasisi za fedha hapa nchini yaani BOT kwani ni wazembe kiasi kwamba watu wamefanya biashara kwa miaka mitatu bila vibali je hivi kweli kama wangelikuwa matapeli si ingelikuwa kilio kikubwa kwa maskini wa tanzania ? hivi wanachotaka nini hasa ?

Hapa ni dhahiri kabisa kwamba wao ndio wanapinga kabisa ile sera ya kuondoa umaskini nchini. MUNGU ametuletea mkombozi ambaye ni DECI watu wamejenga wamepeleka watoto shule wanafanya biashara zao na zinaendelea vizuri, Je nani anaweza akajitokeza na kueleza alivyo nufaika na mabilioni ya JK ? DECI ni neema toka kwa MUNGU nawapa DECI bigup saaaaaaana ! nendeni na mweke mtandao mpaka vijijini.MUNGU awabariki sana viongozi wote wa DECI tuko pamoja tunawa saport na tunawependa sana wala msiogope kelele za mbwa hazimtishi mwenye mbwa kulala

Mjomba JK mimi nakusihi siku moja uitishe mkutano pale viwanja vya jangwani au Biafra (lakini ngoja mvua zipite) halafu katika kadamnasi uulize waliopo nani kafaidika na senti ulizotoa kusaidia maskini na nani kafaidika na DECI utashngaa kuona wenyesuti na vitambi vya hadhi ya juu ndio watasema senti zao ziliwasaidia wakanunua bajaji, na akina sisi tutasemja DECI imetusaidia na leo hii mwanangu anasoma St Mroki Academy na Vyuo vya Mtakatifu Kidevu ila ukiniona wakawaida tu.

BoT na CMSA umakini huu mngeufanya wakati wa kulipa madeni ya EPA walahi leo watu wasingeburuzwa kuaibisha pale Mahakama ya Kisutu kwa michongo ambayo wenyewe mliwapa kuwa kuna fedha andika barua hii na stakabadhi tafuta Kariakoo lete utapata Bilioni 200. Hata mimi ningebuni kampuni ya Kufuga Ndevu na ningesema niliiuzia siri kali tani saba zandevu kwaajili ya kutengeneza maska za wapelelezi.

Mlinong’onezana juu ya pesa za EPA mkala wenyewe sasa mesikia huku kuna neema ya wavuja jasho mmekuja mmechukua mnataka kuwadhulumu na kuwaambia Watumishi wa Mungu wakimbie, ndio… unamaana gani kusema mtu taopeli atakimbia wakati hata hilo wazo hana si unamfundisha wewe. Mtachapwa na wapigakura.

Pia nionavyo mimi nivyema wapigakura waliowanachama wa DECi wakachukua tahadhari hii kuwa huenda kuna utapeli unatendeka mapema maana pia kuna kale kausemi kuwa ‘Lisemwalo lipo na kama halipo laja’ tusijekuwa wakunyooshewa vidole kama wale waliochota shmba la bibi pale BoT katika zao lake lile la EPA na leo wapo Mahakamani.

Hivyo nashauri pia tuitikie kiitikio chetu cha ‘Nayo serikali itakosa wapigakura 2010 x2,’huku tunarudisha mbegu zetu darini zipigwe na moshi na sio kuziweka ghalani (Benki) zikaliwa na Bungubungu na Panya tukaambulia Pumba wakati wa mvua za kwanza. Yes siunajua ukiweka hela Benki zinavyokatwa makato na ukichukua wana kata tofauti na DECI ambayo ukiweka unavuna tu hadi basi. Bure aghali waungwana hunena.

Haya jamani ‘Ada ya Mja Kunena na Muungwana ni Vitendo’sasa mimi ni Mja nimesha Nena Muungwana ni wewe Mwanachama wa DECI, BoT, CMSA na Serikali kutenda ama wanachama kuacha kwanza kuopanda mambo yapoe na ukweli ujulikane au kendelea na hao wengine kuona namna ya kuinusuru DECI.

Mungu wabarijki wavuja jasho wote Tanzania, Mh! Haya na wafuga ndevu kama mimi amina.
Posted by MROKI On Wednesday, April 08, 2009 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo