Nafasi Ya Matangazo

March 15, 2024

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watuhumiwa wanne (4) kwa wizi wa nondo zenye uzito wa takribani tani 5 ambazo zinasadikika kutoka kwenye Mradi wa ujenzi unaoendelea wa uwanja wa ndege wa kimataifa Msalato Jijini Dodoma.

Kufuatia kadhia hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amefika kituo kikuu cha Polisi Dodoma kushuhudia nondo hizo zilizokamatwa jana jioni ambapo gari lililokutwa na vifaa hivyo lipo chini ya uangalizi wa polisi katika kituo hicho.

 Mhe. Senyamule, amelaani vikali wizi unaofanywa na baadhi ya watu wasio na uzalendo kwa mali za Serikali yao kwani ujenzi wa mradi huo ni kwa manufaa ya watanzania kwa ujumla.

“Tumekua tukisisitiza uzalendo, lakini kuna baadhi ya wafanyakazi na wasimamizi wa miradi wanakua wabinafsi. Nitoe onyo kwa wote wanaodhani wanafanya hujuma kuwa Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama tumejipanga kusimamia miradi yote ya kimkakati na hatuwezi kumuangusha Mhe. Rais.

“Hii ni hujuma kubwa kwa Serikali. Polisi na waendesha mashtaka, hakikisheni kesi kama hizi zinachukuliwa kama mfano. Tuwe walinzi wazuri kwa miradi hii na kazi hii itaendelea kufanyika kwenye miradi yote ya Serikali. Dodoma tutahakikisha mali za Serikali zinakua salama” Ameongeza Mhe. Senyamule.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno, amesema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 14 majira ya jioni kwenye eneo la Chikole, Msalato wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T-342 DUP ambalo ndilo lilibeba nondo hizo.

Aidha, amesema kuwa watuhumiwa hao wapo kituo cha polisi huku  wakisubiri uchunguzi ukamilike ndipo wafikishwe mahakamani lakini pia bado wanaendelea kufanya upelelezi ili kuwabaini wote walioshiriki katika kitendo hicho  ili  kuchukuliwa hatua stahiki na kukomesha kabisa vitendo hivyo.
Posted by MROKI On Friday, March 15, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo