Nafasi Ya Matangazo

May 01, 2016

Rais Dk John Pombe Magufuli akiwahutubia mamia ya Wafanyakazi katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zulizofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameshikana mikono na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi TUCTA wakati wakiimba wimbo wa Mshikamano Daima katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma .
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisikiliza maelezo kutoka kwenye banda la Wakala wa Afya na Usalama mahala pa kazi OSHA mkoani Dodoma
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais wa TUCTA Gratian Mukoba wakati alipowasili katika katika viwanja vya Jamhuri Mkoani Dodoma.  BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipunga mkono kuagana na mamia ya wafanyakazi katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza kuwa serikali yake itapunguza kodi katika mishahara ya wafanyakazi kutoka asilimia 11 hadi kufikia asilimia 9 kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017 ili kupunguza mzigo kwa wafanyakazi.

Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo leo tarehe 01 Mei, 2016 wakati akihutubia katika sherehe za maadhimisho ya siku ya siku ya wafanyakazi duniani, zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.

"Napenda kuwataarifa kuwa serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu, nimeamua kupunguza kodi ya mapato ya mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 9, kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017, nikiwa nina mategemeo makubwa waheshimiwa wabunge watapitisha bajeti ya serikali niliyoiwasilisha" Amesema Dkt. Magufuli huku akishangiliwa na maelfu ya wafanyakazi waliojitokeza uwanjani hapo.

Pamoja na uamuzi huo, Rais Magufuli pia amewaahidi wafanyakazi kuwa baada ya kupunguza kodi katika mishahara ya wafanyakazi, serikali yake itafanyia kazi mapendekezo ya kuongeza mishahara.

Katika maadhimisho hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Akson, Rais Magufuli amewataka wafanyakazi kote nchini kushiriki kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 kwa kufanya kazi kwa bidii, kujituma, weledi na uadilifu.

Amesema Mpango wa Maendeleo ya Taifa utagharimu takribani shilingi Trilioni 107 zikiwemo shilingi Trilioni 59 kutoka serikalini, hivyo amewataka wafanyakazi wote kutambua kuwa wanategemewa kuwaongoza watanzania kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa kuchapa kazi.

Aidha, Rais Magufuli amewataka wafanyakazi kuunga mkono juhudi za kuwafichua wanaozalisha wafanyakazi hewa, huku akibainisha kuwa mpaka kufikia jana tarehe 30 Aprili, 2016 jumla ya wafanyakazi hewa waliobainika walikuwa 10,293 ambao kwa mwezi mmoja tu wamelipwa shilingi bilioni 11.6.

"Kwa hiyo kwa mwaka wafanyakazi hewa hawa wamekuwa wakilipwa shilingi 139,239,285,592.92, ukizidisha kwa miaka mitano kama tungekuwa na wafanyakazi hewa, miaka mitano tu, tusiseme miaka kumi au ishirini au kumi na ngapi, miaka mitano tu, manaake wangelipwa shilingi 696,196,427,964.6.

"Hizi bilioni 696 zinatosha kujenga madaraja kama la Nyerere lililopo Kigamboni, madaraja matatu, hizi bilioni 696 zinatosha kujenga flyover zinazojengwa Dar es salaam kwa msaada na mkopo kutoka Japan, zingekuwa saba, hizi bilioni 696 mjiulize kama zingetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi waliopo ndani ya serikali, tungewaongezea mshahara kiasi gani" amesisitiza Rais Magufuli.

Hata hivyo Rais Magufuli amewahakikishia wafanyakazi wote ambao wanatekeleza majukumu yao kihalali kuwa serikali yake itawalinda na kuwatetea huku akitaka wawapuuze wanaodai serikali ya awamu ya tano haiwapendi wafanyakazi.


"Tukumbuke ya kuwa kazi ni utu, kazi sio fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia zetu bali ni fursa nzuri ya kutoa mchango kwa taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho" amesema Dkt. Magufuli.
Posted by MROKI On Sunday, May 01, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo