Nafasi Ya Matangazo

May 12, 2015

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.

MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA KUMUWAKILISHA MAKAMU WA RAIS DKT MOHAMMED GHARIB BILAL KWENYE HARAMBEE YA UCHAGIAJI UJENZI WA MSIKITI WA PATANDI, JIJINI ARUSHA, IJUMAA  MEI 15,2015.
 
Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapenda kuutaarifu umma kuwa shughuli ya Harambee ya kuchangia ujenzi wa Msikiti wa Patandi uliopo wilaya ya Arumeru jijini Arusha ambao umepangwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 15, 2015 na ambayo awali ilitangazwa kuwa mgeni Rasmi katika Harambee hiyo angekuwa Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa itasimamiwa na Mheshimiwa Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa jimbo la Monduli.
 
Mabadiliko haya yanatokana na Mheshimiwa Makamu wa Rais kukabiliwa na majukumu mengine ya Kitaifa na hivyo kutoa ombi maalum kwa Mheshimiwa Edward Lowassa kumuwakilisha katika shughuli hiyo jambo ambalo amekubali.
 
Kufuatia taarifa hii, tunauomba umma na wananchi wote wenye nia njema kushirikiana nasi pamoja na mgeni Rasmi atakayemuwakilisha Makamu wa Rais katika harambee hiyo inayolenga kukusanya fedha ili kukamilisha msikiti huo ambao ulianza kujengwa mwishoni mwa miaka ya 1990.
 
Msikiti wa Patandi upo katika eneo wanalokaa wananchi wenye imani mbalimbali na waumini wanaoutumia msikiti huu, wamekuwa wakijitoa kwa namna nyingi katika kusaidia kujenga mshikamano baina ya jamii zinazowazunguka bila kuwa na vikwazo na pia wamekuwa wakishiriki katika kuwasaidia watoto yatima na wengine wenye uhitaji katika kukabiliana na maisha yao. 
 
Kufuatia dhima hii na mchango huo wa wanajamii wanaoswali katika Msikiti huu, Mheshimiwa Makamu wa Rais ameona na imempendeza kuwa, shughuli hii ya uchangiaji ujenzi isisogezwe mbele kumsubiri bali iendelee kwa kuwa anaamini Mheshimiwa Lowassa ni mzoefu katika kufanikisha shughuli za aina hii na kwamba mchango wake katika jamii hasa shughuli za harambee ni wa kutiliwa mfano. Tunawakaribisha sana kushirikiana naye katika kufanikisha Harambee hii. Kumbukeni kutoa ni moyo na wala si utajiri!
 
Imetolewa na:  Boniphace Makene
     Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais
Dar es Salaam: 12 Mei 2015
Posted by MROKI On Tuesday, May 12, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo