Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Wananchi waliojitokeza kujionea maendeleo ya ujenzi wa kongani ya viwanda ya kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited) wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani leo tarehe 16 Oktoba, 2026.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Wananchi wa Bagamoyo katika Viwanja wa Shule ya Msingi Majengo vilivyopo mkoani Pwani.
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu
Nchemba, ameagiza kukamilishwa haraka kwa uthamini wa maeneo yanayohitajika kwa
uwekezaji katika Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo ili wananchi walipwe
fidia na miradi iendelee bila migogoro.
Ametoa maelekezo hayo leo,
Ijumaa, Oktoba 16, 2026, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kongani ya viwanda
ya kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited), wilayani Bagamoyo, mkoani
Pwani.
Dkt. Mwigulu ameelekeza Ofisi ya
Rais, Mipango na Uwekezaji na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya
Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi pamoja na uongozi wa mkoa na wilaya kukamilisha uthamini huo. Amesema
serikali imeweka chanzo mahususi cha fedha za kulipa fidia kwa wananchi
wanaopisha miradi ya maendeleo.
“Fanyeni uthamini, wanaoachia
maeneo kupisha uwekezaji walipwe haki yao,” amesema.
Amesisitiza kuwa baada ya malipo
ya fidia, maeneo hayo yapatiwe hati za kisheria na kuwekewa mipaka inayoeleweka
ili kuzuia uvamizi. Akijibu maelezo kuwa uthamini ulisimama kutokana na
tahadhari za mvua za El Niño, ameagiza kazi iendelee huku tahadhari
zikizingatiwa.
“Tuchukue tahadhari huku
tukiendelea na kazi,” amesema.
Kuhusu vijana, Waziri Mkuu
ameagiza kuharakishwa kwa maandalizi ya eneo la ekari 50 lililotengwa kwa ajili
ya mabanda ya viwanda na kituo cha mauzo ya nje. Amesema upatikanaji wa maeneo
ya uzalishaji na biashara ni muhimu katika kuwawezesha vijana kushiriki katika
uchumi na kutengeneza ajira.
Dkt. Mwigulu amesema kufikia
malengo ya Dira ya Taifa 2050 kunahitaji ushiriki mpana wa wananchi na sekta
binafsi imara. Amehimiza kuanzishwa kwa shughuli mpya za uzalishaji
zitakazopanua ajira na vyanzo vya mapato ya serikali, huku akisisitiza kuwa
utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa wakati unalinda haki za wananchi na kuwezesha
uwekezaji kufanyika kwa amani.
Aidha, amepongeza maendeleo ya
kongani hiyo, akisema yanaonesha hatua za utekelezaji wa maono ya Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi wa uzalishaji.
Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, amesema uwekezaji wa ndani na nje
una mchango muhimu katika kukuza uchumi kupitia ajira kwa vijana, mauzo ya nje,
upatikanaji wa fedha za kigeni na teknolojia za kisasa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
TISEZA, Anna Limo, amesema Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo lina wawekezaji
36, wakiwemo wapya 25 waliopewa maeneo kuanzia Desemba 2025. Amesema eneo la
hekta 5,135.22 bado halijalipiwa fidia, huku sehemu yake ikiwa ilifanyiwa
uthamini mwaka 2009.
Kuhusu eneo la vijana, amesema
mpango huo unalenga kuwapatia mabanda ya viwanda kwa gharama nafuu, miundombinu
ya msingi, usaidizi wa leseni na vibali, pamoja na masoko ya bidhaa ndani na
nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Hongwang Tanzania, Sophia Su, amesema kampuni hiyo imepanga kutumia
dola za Marekani milioni 150 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu na
uendelezaji wa eneo, huku karibu dola za Marekani milioni 30 zikiwa zimetumika
hadi Oktoba 2026. Amesema kiwanda cha kuunganisha malori kinatarajiwa kuanza
uzalishaji wa kibiashara kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Ameongeza kuwa mradi umetoa ajira
170 kwa Watanzania na unatarajia kufikisha takribani ajira 400 ifikapo mwisho wa
mwaka, huku kampuni ikitoa kipaumbele kwa wazabuni wa ndani. Naye Mkuu wa Mkoa
wa Pwani, Stanislaus Nyongo, amesema mkoa utaendelea kushughulikia uvamizi wa
ardhi na kuimarisha miundombinu ili kuweka mazingira bora kwa wawekezaji.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akipokea maelezo ya ujenzi wa kongani ya viwanda ya kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited) kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hongwang Tanzania, Sophia Su kilichopo wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani leo tarehe 16 Oktoba, 2026.
0 comments:
Post a Comment