Wananchi wanaotembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) wanapata fursa ya kujifunza mchango wa mashamba ya miti ya kupandwa katika kukuza uchumi wa viwanda na biashara ya mazao ya misitu nchini.
Katika banda hilo, TFS inaonesha jinsi mashamba ya miti yanavyotoa malighafi kwa viwanda mbalimbali vinavyozalisha mbao, samani, karatasi na bidhaa nyingine za misitu, huku yakichangia uhifadhi wa mazingira na kuongeza ajira.
Mbali na hilo, wageni wanapata nafasi ya kujionea uzalishaji wa mianzi na kufahamu matumizi yake katika ujenzi, utengenezaji wa samani, bidhaa za ubunifu na uhifadhi wa mazingira.
Wataalamu wa TFS pia wanatoa elimu kuhusu mbinu bora za upandaji na utunzaji wa miti, uvunaji endelevu, pamoja na taratibu za kufanya biashara ya mazao ya misitu kwa kuzingatia sheria na kanuni.
Kupitia maonesho hayo, TFS inawahimiza wananchi, wawekezaji na wafanyabiashara kutembelea banda lake ili kupata ushauri wa kitaalamu, kufahamu fursa zilizopo katika sekta ya misitu na kushiriki katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.










0 comments:
Post a Comment