Maridhiano baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Alliance For Change and Transparency (ACT-Wazalendo) kuelekea uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, umepongezwa kwani umezingatia maslahi ya nchi ambayo ni muhimu kuliko maslahi binafsi ya wanasiasa.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa Viti Maalum CCM na Mwenyekiti Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, Julai 9, 2026, Jijini Dodoma.
Akitoa maoni yake baada ya kumalizika hafla hiyo ya Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa baina ya vyama hivyo, Chatanda amesema, Wazanzibar wameshasahau siasa za chuki, kipaumbele chao sasa ni umoja, mshikamano na maendeleo.
"Wazanzibar ni watu rahimu sana, wao wanataka amani, mshikamano na maendeleo na kitendo cha vyama hivi viwili kufikia muafaka, ni ishara ya ukomavu wa kisiasa na kuzingatia maslahi ya nchi," amesema Chatanda.
Aidha, amesema maridhiano hayo yana maana kubwa katika kuhakikisha SUK inaundwa kwa ukamilifu wake kwani SUK ndiyo mwelekeo wa siasa za Zanzibar katika uundwaji wa serikali.
Sambamba na hilo, amesema ni muhimu kwa wananchi na wanasiasa wa Zanzibar kumpa ushirikiano Rais Dk. Hussein Mwinyi ambaye amejipambanua kuwa kiongozi mchapakazi, msikivu na mpenda maendeleo kwa wananchi wake.
"Wazanzibar wana Rais mchapakazi na mwenye maono makubwa ya maendeleo, wananchi wanapaswa kumpa ushirikiano na kuhakikisha Zanzibar inasonga mbele kwa kasi," amesisitiza.
Katika hafla hiyo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa, maridhiano hayo si udhaifu bali ni ukomavu wa kisiasa na unafungua ukurasa mpya wa umoja, amani, utulivu na mshikamano kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
"Uungwana hautufunzi kiburi na kutosikilizana. Wananchi wetu hawahitaji vurugu wala mivutano ya kisiasa isiyoisha. Wananchi wetu wanahitaji amani, usalama na utulivu," amesema Rais Dk. Samia








0 comments:
Post a Comment