Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaka Halmashairi ya Jiji la Mwanza kwa upande mmoja na Wananchi hususani wa Kata ya Luchelele kwa upande mwingine kuwa na utashi wa kumaliza migogoro ya ardhi kwa kusikilizana huku akisisitiza kuwa kama utashi haupo pande zote mbili mgogoro hauwezi kuisha.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo mapema leo Mei 19, 2026 katika Mkutano wa hadhara alioufanya katika Kata ya Luchelele ambapo amesema kuwa.
" Jiji la Mwanza ifike mahala tuseme migogoro ya ardhi Luchelele sasa basi, Jiji ni sehemu ya mgogoro kwa kutolipa fidia kwa wakati na wananchi kwa kutokubali fidia na kutopokea maelekezo kwa upande mwingine huku akitanabaisha kuwa ili kumaliza mgogoro kila upande uwe na utayari" amesisitiza Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameongeza kuwa ni muhimu kumaliza migogoro hii kwani inazuia maendeleo na hakuna muwekezaji anayeweza kukubali kujenga eneo lenye mgogoro.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makiragi amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Saidi Mtanda kwa kuendesha Mkutano huo na kuwataka wana Luchelele kutumia fursa hiyo adhimu kuwasilisha kero zao mbalimbali ili zipate utatuzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Kata ya Luchelele wakiendelea kutoa kero zao, wamemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuja kuwasikiliza wakiwa na matumaini makubwa kuwa sasa kero zao hususani za ardhi zinaenda kutatuliwa.
Awali akisoma taarifa ya Mradi wa viwanja Luchelele kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Afisa ardhi Mteule wa Jiji la Mwanza Ndg. Abenance Kamomonga ameeleza changamoto zinazochangia migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kutojitokeza wakati wa ukaguzi hivyo kutofanyiwa tathmini na kutoshiriki zoezi la uhakiki sambamba na kudai fidia mara mbilimbili na kupendekeza kuwa viongozi wa serikali ya mitaa wasijihusishe na masuala ya ardhi bila kuwashirikisha wataalamu wa ardhi na wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano.









0 comments:
Post a Comment