Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji ametembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika maonesho ya Wizara ya Maliasili na Utalii yanayoendelea kwenye viunga vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
Mhe. Dkt. Kijaji, akiambatana na viongozi mbalimbali wa wizara hiyo, alifanya ziara hiyo mara baada ya kuwasilisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni mapema leo.
Katika ziara hiyo, Waziri alipata fursa ya kujionea na kupata maelezo kuhusu shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotekelezwa kupitia sekta ya misitu nchini, ikiwemo uhifadhi wa misitu, utalii wa mazingira, uzalishaji wa mazao ya misitu pamoja na mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, banda la TFS limeendelea kuvutia wadau mbalimbali wanaotembelea maonesho hayo kutokana na ubunifu na maonesho ya shughuli za uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.
Pamoja na mambo mengine, banda hilo pia linatoa huduma ya tiba ya kudungwa na nyuki (Api-Therapy) bure kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo. Huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za TFS kuelimisha Watanzania kuhusu manufaa ya uhifadhi wa mazingira kupitia matumizi ya tiba za asili zinazotokana na rasilimali za misitu.
Kwa mujibu wa Mhifadhi wa TFS ambaye ni Afisa Nyuki kutoka Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Vikindu, Brenda Mwakipesile alisema huduma hiyo inalenga kusaidia kuimarisha kinga ya mwili, kupunguza maumivu ya viungo, kuboresha mzunguko wa damu pamoja na kusaidia afya ya akili.
“Tumeileta huduma hii bure kwa wananchi ili kuwaonesha kuwa uhifadhi wa misitu hauishii kwenye miti pekee, bali pia unaweza kuzaa tiba za asili ambazo ni salama na zenye manufaa ya kiafya,” alisema Mhifadhi Brenda.
Katika maonesho hayo, viongozi mbalimbali waliotembelea banda la TFS leo pia walipata huduma ya kudungwa na nyuki kama sehemu ya kujionea kwa vitendo huduma hiyo ya tiba asilia, kama wanavyoonekana pichani.












0 comments:
Post a Comment