Nafasi Ya Matangazo

December 18, 2025






Na Mwandishi Wetu, Mahenge
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amezitaka Ofisi za Madini kote nchini kuimarisha utoaji wa elimu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuhusu uzalendo na umuhimu wa kulipa kodi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha nidhamu katika sekta ya madini.

Dkt. Kiruswa ametoa kauli hiyo leo Desemba 18, 2025 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Kimadini Mahenge, ambapo ametembelea na kukagua shughuli za uchimbaji madini katika eneo la Epanko, kwenye mgodi unaoendeshwa na kampuni za Ruby International na Flanone Ltd. Katika ziara hiyo, pia amepata fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wa madini.

“Ofisi za Madini zina wajibu wa kuwajengea wachimbaji na wafanyabiashara wa madini uelewa kuhusu ulipaji kodi na uzalendo, ili kila mmoja atimize wajibu wake katika kuchangia maendeleo ya taifa,” amesema Dkt. Kiruswa.

Akizungumzia changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wachimbaji wadogo, Dkt. Kiruswa amesema Wizara ya Madini imeanzisha programu ya Mining For A Brighter Tomorrow (MBT), itakayosaidia kutoa mitaji na vifaa vya kazi kwa wachimbaji, hususan vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum.

Aidha, Naibu Waziri huyo amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa madini ya vito katika Soko Kuu la Madini ya Vito la Mkoa wa Kimadini Mahenge, ambapo amewataka kuachana na vitendo vya utoroshaji wa madini na kuzingatia kikamilifu Sheria, Taratibu na Kanuni zinazosimamia biashara ya madini.

Amesisitiza kuwa mfanyabiashara yeyote atakayebainika kujihusisha na utoroshaji wa madini atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufungiwa leseni na kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Simba, amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kutembelea wilaya hiyo na kusikiliza changamoto za wachimbaji, akisema sekta ya madini ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wilaya kupitia ajira na mapato ya Serikali.

Simba amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Ofisi ya Madini kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini na kulinda rasilimali za taifa.

Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Kimadini Mahenge, ambapo Afisa Madini Mkazi, Jonas Mwano, aliwasilisha taarifa ya mapato na maendeleo ya sekta ya madini ya mkoa huo.
Posted by MROKI On Thursday, December 18, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo