WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemwagiza Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI) awaandikie barua Wakuu wote wa Mikoa ili waunde timu za ukaguzi wa majengo na miradi kwenye mikoa yao kama njia ya kukabiliana na wakandarasi wanaokiuka makadirio ya gharama za ujenzi (BOQ) wa miradi ya Serikali.
"Yuko Mhandisi ambaye huwa anakagua miradi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru. Wakuu wa Mikoa wote wawe na timu za vijana wa aina hiyo, ili wasiuziwe mbuzi kwenye gunia. Iwe ni utamaduni wa Serikali kufanya ukaguzi wa aina hiyo," amesema Waziri Mkuu.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Desemba 21, 2025) wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya za Ruangwa na Nachingwea, mkoani Lindi akiwa katika ziara ya siku tatu ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Waziri Mkuu amesema kuna baadhi ya miradi ambayo wakandarasi wake hawafuati BOQ. "Unakuta BOQ inataka nondo za mm 16 lakini mkandarasi anaweka za mm 12. Kuna mahali zinatakiwa nondo sita, yeye anaweka nondo nne. Jengo likikamilika, huwezi kuona na kulinganisha makubaliano ya BOQ. Nimeelekeza kila mkoa uwe na timu ya wataalamu wa kukagua miradi ya Serikali."
"Mikoa yote wawe na vitengo hivi na wawe pia na vifaa vya kuchunguza majengo na miradi mingine badala ya kusubiri uchunguzi unaofanywa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru. Vitengo hivyo kazi yao ya kila siku ni kufuatilia miradi ili kubaini maeneo ambako Serikali imetoa fedha na hazijatumika vizuri ili tuweze kuchukua hatua," amesisitiza.
Mapema, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Lindi-Ruangwa- Nachingwea uliojengwa kwenye kijiji cha Chimbila A wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Mradi huo ambao chanzo chake kinatoka mito ya Nyangao na Chilua wilayani Lindi, unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pindi utakapokamilka, utanufaisha vijiji 56 katika Wilaya za Ruangwa (vijiji 34), Wilaya ya Nachingwea (vijiji 21) na Wilaya ya Lindi (Kijiji 1).
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa RUWASA, Mhandisi Walter Kirita amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 119 na hadi sasa wameshalipa sh. bilioni 49 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 67 ya utekelezaji.
Mradi huo umeanza kutekelezwa Februari, 2023 na awamu ya kwanza (Lot 1) inatarajiwa kukamilika Juni, 2026. Hata hivyo, Mhandisi Kirita alimweleza Waziri Mkuu kwamba ifikapo Februari, 2026 baadhi ya vijiji vitaanza kupata huduma ya maji.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, Dkt. Mwigulu alisema ameridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi ambayo imefikiwa. “Hivi ndivyo Rais Dkt. Samia anataka kuona namna kazi inavyofanyika. Hapa tumeona asilimia ya utekelezaji ni kubwa kuliko fedha zilizotolewa hadi sasa. ”
Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu mstaafu, Kassim M. Majaliwa kwa kuasisi mradi huo na kufuatilia fedha za mradi kila mara.










0 comments:
Post a Comment