Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema anaamini maagizo yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko wakati wa ufunguzi wa michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) iliyofanyika tarehe 7 septemba, 2025 yatatekelezwa na waajiri.
Dkt. Biteko alitoa maagizo ya wakuu wa wizara na taasisi kuruhusu timu zao kushiriki kwenye michezo hii, ambayo inahimarisha afya, na kuongeza tija na mahusiano baina ya watumishi wa sehemu mbalimbali.
Akizungumza katika ufungaji wa michezo hiyo iliyoanza tarehe 01 Septemba na kuhitimishwa Septemba 16, 2025 Mhe. Mtanda amesema anatarajia maelekezo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi, lakini ametoa wito kwa wizara na taasisi zote kuwa na mipango endelevu ya kwa ajili ya michezo ya SHIMIWI.
“Bila shaka wakati wa ufunguzi wa michezo hii Dkt Biteko alitoa maelekezo mblimbali kwa viongozi mbalimbali wa serikali, wizara, taasisi na SHIMIWI, naamini maelekezo haya yote yatakwenda kutekelezwa,” amesema Mhe. Mtanda.
Amesema michezo hii imeleta faida kubwa kwa mkoa wa Mwanza, kwani watumishi zaidi ya 3353 wameweza kushirikiana na wenyeji katika huduma mbalimbali za kijamii, wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wakubwa wameweza kunufaika pia.
Halikadhalika amepongeza uongozi na waandaaji wa michezo ya SHIMIWI na wenyeji mkoa wa Mwanza chini ya Ofisi ya Katibu Tawala, waamuzi, wasimamizi na viongozi wa klabu kwa kuwasimamia washiriki wote na ushirikiano huo umefanikisha michezo hii kwa umahiri mkubwa, ambapo pia awali uongozi uliandaa mafunzo na mkutano wa maandalizi ya michezo hii, ambayo vimesaidia kufanikisha kufanyika vyema.
“Nipende kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufikisha tamati ya michezo hii, na ninatoa pole nyingi kwa wanamichezo na familia kwa ujumla kwa kuondokewa na mwenzetu Bw. Chiza Joseph aliyekuwa Afisa Michezo kutoka Lindi, aliyefariki akiwa kwenye kituo cha michezo hapa Mwanza,” amesema Mhe. Mtanda
Ameutaka uongozi wa SHIMIWI kushirikisha makundi maalum ya watumishi kushiriki michezo hii, ambapo amefarijika kwa washiriki kusaidia jamii kwa kutoa misaada kwa wahitaji yenye thamani ya Tshs Milioni 14,866,500, na pia amewapongeza washiriki kwa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo jijini Mwanza na mikoa ya jirani.
“Endeleeni kutekeleza maelekezo ya michezo hii kwa kujenga mtandao mzuri wa ushirikiano na mahusiano mazuri na muone umuhimu wa watumishi kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi mahala pa kazi badala ya kusubiri SHIMIWI pekee,” amesema Mhe. Mtanda.
Hatahivyo, akimekumbusha kupitia nukuu ya Mhe. Dkt. Biteko ya wakati wa ufunguzi wa michezo hii kuwakumbusha wadau wa michezo nchini, kuandaa na kuitunza miundombinu ya viwanja vya michezo ikiwemo ya netiboli, mpira wa miguu, riadha, mpira wa wavu, na michezo mingine.
Amewakumbusha watumishi walioshiriki michezo hii kuwa wanawajibu wa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Awali Makamu Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Michael Masubo amesema michezo ya mwaka huu 2025 imeshirikisha wizara 21, mikoa 23, wakala na taasisi za serikali 22, ambapo amelishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni na Sanaa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa miongozo yao na ushirikiano wao katika kuandaa michezo hii, pamoja na uongozi wa jiji la Mwanza kwa ushirikiano wao mkubwa.
Bw. Masubo ameendelea kuwaomba waajiri waweze kutenga fedha kwa ajili ya ushiriki wa watumishi kwenye michezo hii na kuendeleza michezo mahala pa kazi, ambapo huwajengea afya na umahiri katika utendaji wao wa kazi.
Bw. Masubo amesema changamoto zinazojitokeza hutatuliwa kwa kutumia vikao halali vilivyoainishwa kwenye katiba ukiwemo mkutano mkuu unaoweka miongozo na kuondoa mianya yenye kusababisha changamoto na pia hutatuliwa kwenye vikao halali.
Amesema watumishi wote wamejiandikisha na Oktoba 29 watashiriki kwenye uchaguzi mkuu wa kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi Savera Salvatory, ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, amewapongeza weenyeji jijini la Mwanza kwa ushirikiano wao mkubwa na kutokana na mashindano haya yamekuwa chachu ya kukuza uchumi wa jijini hili.
“Ninaupongeza uongozi wa SHIMIWI kwa kuratibu mashindano haya vizuri kwa kuwa walikuwa na vilabu shiriki zaidi ya 66 sio jambo rahisi wanastahili pongezi, hatahivyo Wizara imepata taarifa za baadhi ya matukio yakiwemo ya uendeshaji katika maamuzi, kubadilishwa kwa ratiba na rufaa zilizokatwa,basi natoa rai kwa viongozi michezo hii kuendesha michezo hii kwa haki wahakikishe ushindi unapatikana kutokana na matokeo ya uwanjani na wakae na viongozi wa klabu kwa ajili ya kufanya tathmini ya michezo hii ili kutatua changamoto zilizojitokeza,” amesema Bi. Saveta.
Aidha, amekumbushia waajiri kuhusu maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan agosti 22, 2025 kwa kuzitaka wizara, taasisi kushiriki michezo ya SHIMIWI ili kuimarisha afya zao, hivyo wizara ya habari inapenda kuona maelekezo haya yanatekelezwa kwani taasisi ni klabu halali zinazosajiliwa na Baraza la Michezo la Taifa kwa ajili ya kuendesha michezo.
Pia amezitaka klabu kufuata katiba zao kwa kufanya vikao, kufanya uchaguzi, kuendesha vikao vyote vya kamati tendaji, na amewapongeza waajiri wote walioleta timu kwenye michezo hii.















0 comments:
Post a Comment