Wizara ya Madini kwa kushirikiana na taasisi zake inaendelea kutoa elimu ya kina kuhusu shughuli za madini katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Kupitia banda la Wizara hiyo, wananchi, wawekezaji na wanafunzi wanapata fursa adhimu ya kujifunza kwa undani kuhusu sekta ya madini nchini, kuanzia shughuli za uchimbaji, uchenjuaji, usimamizi wa mazingira, hadi masuala ya usafirishaji wa madini na masoko ya madini.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mjolojia kutoka Wizara ya Madini, Neema Masinde, amesema kuwa lengo la ushiriki wa Wizara na taasisi zake ni kuhakikisha wananchi wanaelewa mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuwapa maarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za sekta hiyo.
“Tunatoa elimu ili kuwahamasisha wananchi washiriki kwa tija katika sekta hii muhimu, kwani ni miongoni mwa sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa (GDP) pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania,” amesema Masinde.
Maonesho ya Sabasaba mwaka huu yamevutia washiriki kutoka zaidi ya nchi 40, huku banda la Wizara ya Madini likitajwa kuwa miongoni mwa mabanda yaliyovutia idadi kubwa ya wageni kutokana na mvuto wa sampuli mbalimbali za madini na elimu ya moja kwa moja inayotolewa na wataalam waliobobea.
0 comments:
Post a Comment