Nafasi Ya Matangazo

May 21, 2025

 








NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amewataka wasanii, wabunifu na wadau wa sekta ya sanaa nchini kuhakikisha wanasajili kazi zao za ubunifu ili kulinda haki zao na kunufaika kifedha kupitia mapato halali yanayotokana na matumizi ya kazi hizo, hasa katika mazingira ya sasa ya kidijitali ambapo wizi wa kazi za sanaa umeongezeka.

Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo leo Mei 21, 2025 alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani ambapo ameeleza kuwa usajili wa haki za kazi za ubunifu si suala la hiari bali ni nyenzo muhimu ya kiuchumi, hasa kwa taifa linalojipambanua kuelekea uchumi wa viwanda unaotegemea maarifa.

“Miliki bunifu si tu hati za kisheria, bali ni silaha ya kiuchumi katika dunia ya sasa. Tunaposhindwa kuzilinda, tunapoteza mapato, ajira na fursa za maendeleo. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa kazi za wasanii na wabunifu zinalindwa ili ziwasaidie kiuchumi,” amesema Dkt. Jafo.

Akitolea mfano, Dkt. Jafo amewataja baadhi ya wasanii waliogeuza majina yao ya kisanii kuwa chapa za kibiashara kama Nandy (Sha Sha), Juma Jux (African Boy), Diamond Platnumz (Chegu), Harmonize (Konde), Alikiba (Kiba) na Hamisa Mobetto (Mobetto Style Boutique), akisema kuwa ni mifano hai ya ubunifu uliosajiliwa na kufanikisha mapato halali.

Amepongeza pia taasisi za BRELA na COSOTA kwa juhudi zao za kusaidia wasanii kupata haki zao, lakini aliwataka kuongeza nguvu zaidi katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na kazi za sanaa, hususan katika majukwaa ya kidigitali kama Spotify, YouTube na Boomplay, ambako wasanii wengi wa Kitanzania wameendelea kupata umaarufu lakini si wote wanaonufaika kifedha.

“Huu ni wakati wa COSOTA kuweka mkazo mkubwa katika ufuatiliaji na ukusanyaji wa mapato ya kidigitali. Wasanii wetu wanastahili kulipwa ipasavyo. Hili si tu suala la sheria, bali ni la maadili na haki,” amesema Dkt. Jafo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali za serikali, kama vile BRELA, COSOTA, BASATA na TCRA, akisema serikali inaendelea kupitia na kuboresha sheria za Miliki Bunifu na pia kujiunga na mikataba ya kimataifa ili kuboresha ulinzi wa kazi za wabunifu wa Tanzania ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Jafo amepongeza uzinduzi wa Tuzo za Taifa za Miliki Ubunifu (NIPA) zilizoandaliwa kwa mara ya kwanza na BRELA, akisema ni hatua chanya ya kutambua na kuhamasisha ubunifu unaochangia maendeleo ya nchi. 

“Tuzo hizi si tu heshima kwa wabunifu, bali ni kichocheo cha uvumbuzi mpya utakaosaidia kutatua changamoto za kijamii,” amesema.

Kwa wabunifu ambao hawakupata tuzo mwaka huu, amewahimiza kutokata tamaa bali waendelee kubuni kwa kuzingatia usajili na ulinzi wa kazi zao ili zisichukuliwe bila idhini.

Waziri huyo pia ameipongeza WIPO na ARIPO kwa kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha uelewa na ulinzi wa haki za ubunifu, huku akitoa rai kwa wasanii kuwa mabalozi wa amani hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

“Hatutakuwa na muziki wala ubunifu kama hakuna amani. Wasanii wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuihubiri,” amesema.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wabunifu kutoka sekta mbalimbali waliopata fursa ya kuonyesha kazi zao zikiwemo nguo, michoro, programu za kiteknolojia, na vifaa vya nishati jadidifu. 

Awali Dkt. Jafo alitembelea mabanda hayo na kupongeza wabunifu kwa kuonyesha kazi zenye ubunifu wa hali ya juu unaoakisi utamaduni wa Kitanzania.

Katika hotuba yake, Waziri Jafo amegusia pia kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu, akieleza kuwa sera hiyo itasaidia kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu, kuimarisha mifumo ya usajili, na kuleta tija katika ufuatiliaji wa kazi za ubunifu nchini.

“Sera hii ni dira kwa taifa. Hatutaki mbunifu atoe jasho kubuni halafu baadaye abaki analia kwa sababu kazi yake imeibiwa. Tunataka wabunifu wafaidike ipasavyo,” amesema.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, akizungumza katika maadhimisho hayo, ameeleza kuwa licha ya mafanikio ya muziki wa Tanzania kufika mbali kimataifa, changamoto ya kutosajili kazi bado ni kubwa. 

“Wasanii wengi hawajasajili kazi zao, na hivyo wanapoteza mapato makubwa. Muziki si burudani tu – ni biashara inayohitaji ulinzi wa kisheria,” amesema.

Amefafanua kuwa BRELA sasa imepanua huduma zake na wasanii wanaweza kujisajili mtandaoni kupitia mfumo wa Online Registration.

Ameongeza kuwa elimu kuhusu miliki bunifu inaendelea kutolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo COSOTA, taasisi za elimu na mashirika ya maendeleo.

“Wapo wasanii wa zamani ambao nyimbo zao bado zinapigwa hadi leo, lakini hawapati hata senti kwa sababu hawakuzisajili. Hili ni pigo kwa familia zao,” amesema Nyaisa, huku akihimiza vijana kutumia maarifa yao kubuni bidhaa au huduma zitakazosaidia jamii na kuinua maisha yao.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA ameeleza kuwa tangu mwaka 2001 kazi zaidi ya 3,200 za muziki zimesajiliwa na wasanii zaidi ya 395 wameandikishwa. Kwa mwaka 2023 pekee, zaidi ya Shilingi bilioni 2.7 zilitolewa kwa wasanii kama malipo ya mrabaha.

Hata hivyo, amekiri kuwa idadi hiyo bado ni ndogo ukilinganisha na kazi zinazozalishwa kila mwaka. Alihimiza kuwepo kwa sheria kali zaidi dhidi ya wizi wa kazi za ubunifu na kuongeza ufuatiliaji wa matumizi ya kazi hizo kwenye majukwaa kama YouTube, Spotify na TikTok.

Siku ya Miliki Ubunifu Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha umuhimu wa ulinzi wa kazi za ubunifu katika kuchangia maendeleo endelevu. Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa: “Muziki na Miliki Bunifu: Sikiliza Mdundo Wamiliki Ubunifu”, ikisisitiza umuhimu wa kutumia maarifa, ubunifu na teknolojia kama nguzo ya kujenga uchumi wa kisasa.

Dkt. Jafo amehitimisha kwa kusema: “Tanzania ya viwanda inahitaji wabunifu waliothubutu kusajili kazi zao na kuzilinda kwa ujasiri. Tujenge taifa linalothamini ubunifu kama urithi wa kiuchumi na kijamii.”
Posted by MROKI On Wednesday, May 21, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo