Na Mwandishi wetu, Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Reuben Lekashingo, amehitimu shahada ya uzamivu (Doctorate in Business Administration) kutoka Georgia State University – Robinson College of Business nchini Marekani. Aliporejea nchini, Dkt. Lekashingo alipokelewa kwa shangwe na pongezi kutoka kwa menejimenti na watumishi wa Tume ya Madini katika ofisi za Makao Makuu, Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa, Dkt. JR Lekashingo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki katika usimamizi wa Sekta ya Madini, jambo lililomhamasisha kujiendeleza kielimu.
Alisema kuwa uongozi wa Rais Samia umeweka mazingira rafiki yanayohamasisha maendeleo binafsi na ya kitaaluma, jambo lililompa motisha wa kutimiza ndoto yake ya kielimu.
Aidha, Dkt. JR Lekashingo aliwapongeza viongozi wengine kwa msaada na motisha waliompa, wakiwemo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, aliyekuwa Waziri wa Madini wakati alipoanza masomo yake ya uzamivu, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Naibu Katibu Mkuu, Msafiri Mbibo, na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
“Nawashukuru sana viongozi na watumishi wa Tume ya Madini kwa kuniunga mkono na kunitia moyo wakati wa safari yangu ya kielimu. Ushirikiano wenu umenipa nguvu ya kufikia ndoto yangu bila kuathiri majukumu yangu ya kikazi,” alisisitiza Dkt. Lekashingo.
Dkt. JR Lekashingo pia aliwapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na watumishi wote wa Tume ya Madini kwa jitihada zao za kuboresha ukusanyaji wa maduhuli, hali iliyosaidia kuchangia kwa asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa, hatua inayoakisi maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
Aliendelea kusema kuwa, atahakikisha anatumia ujuzi mpya katika usimamizi wa Sekta ya Madini sambamba na kuwa mfano bora kwa watumishi anaowasimamia ndoto yake ikiwa ni Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa Tume ya Madini, Nsajigwa Kabigi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji, alimpongeza Dkt. JR Lekashingo kwa hatua kubwa ya kuhitimu masomo yake na kuongeza kuwa uongozi wa Tume ya Madini na watumishi wote, wataendelea kumpa ushirikiano kwa ajili ya mafanikio zaidi ya Sekta ya Madini nchini.
Watumishi wa Tume ya Madini kwa nyakati tofauti walimpongeza Dkt. JR Lekashingo kwa mafanikio hayo, wakiongeza kuwa hatua yake imeleta hamasa kwa wengine kujiendeleza kitaaluma ili kuimarisha zaidi usimamizi wa sekta hii muhimu kwa uchumi wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment