May 31, 2025
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limeihakikishia Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa itaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa Mei 29, 2025 alikutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wa Japan cha Urafiki na Afrika (Africa Union Parliamentarians Friendship) Mheshimiwa Ichiro Aisawa, kwenye Ofisi za Bunge la Japan.
May 29, 2025
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasili katika viwanja vya Bunge mapema Mei 29, 2025 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (wa kwanza kushoto) akifuatilia wasilisho la Hotuba ya Makadirio na Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026, Mei 29, 2025 jijini Dodoma. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu wake Bi. Lucy Kabyemera na kulia ni Kamishna wa Ardhi Bw. Nathaniel Mathew Nhonge.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasilisha Hotuba ya Makadirio na Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026 Mei 29, 2025 jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, Wizara ya Ardhi inakusudia kuanzisha Kamisheni ya Ardhi ambayo itaweka mfumo mmoja wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi katika ngazi zote hatua aliyoieleza kuwa, itasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya sekta.
“Tumechelewa sana kuwa na Kamisheni ya Ardhi, tumechelewa sana kuhakikisha nchi yetu imepangwa na kupimwa. Kamisheni itasaidia uwajibikaji katika mamlaka zote katika shughuli za sekta ya ardhi zinatekelezwa katika ngazi ya Wizara, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa” amesema Waziri Ndejembi.
Aidha, Waziri Ndejembi ameweka wazi kuwa, ili kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, Wizara ya Ardhi imependekeza kuwepo Sheria ya Milki itakayoanzisha Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Milki (RERA).
Mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kuunda mfumo madhubuti wa usimamizi wa sekta ya milki, kuratibu na kutunza taarifa wadau na soko la milki, kusimamia tija na ufanisi wa wataalam wa sekta pamoja na kudhibiti uhalifu wa utakatishaji fedha haramu.
“Natoa wito kwa wadau wote wa sekta ya milki kuhakikisha wanasajiliwa na kutambuliwa na Serikali ili kuimarisha ushirikiano na ukuaji endelevu wa sekta hii muhimu katika uchumi wa nchi” amesema Waziri Ndejembi.
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa jimbo la Mtera mkoa wa Dodoma Mhe. Livinstone Lusinde ameitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendelea kuwahudumia watanzania kwa kutenda haki ili kuacha alama kwa watu kupata haki zao.

Na Mwandishi wetu, Pwani
Kiwanda cha kuzalisha unga wa chokaa (ground calcium carbonate) cha Stalick, kilichopo katika Kata ya Msoga, Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, kimeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii inayozunguka eneo hilo kwa kutoa ajira na kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii.
Akizungumza kupitia mahojiano maalum, Meneja wa Kiwanda hicho, Expeditor Mlanzi, amesema kuwa zaidi ya asilimia 98 ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ni vijana kutoka maeneo ya jirani, jambo ambalo limeleta mwamko mpya wa kiuchumi kwa familia na jamii kwa ujumla.
"Ajira hizi zimekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na jamii, kwani vijana wengi sasa wanapata kipato cha uhakika kupitia nafasi walizopata katika kiwanda chetu," amesema Mlanzi.
Mbali na ajira, kiwanda hicho kimekuwa kikitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR). Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa darasa na kisima cha maji katika Shule ya Msingi Rubani, pamoja na uboreshaji wa vyoo katika Shule ya Msingi Changa.
Aidha, Mlanzi ameongeza kuwa kiwanda kinanunua malighafi na kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo ya karibu kama Ukerewe, Rubaya, Msolwa na Nkuta, hali inayochochea zaidi mzunguko wa fedha na uchumi katika maeneo hayo.
"Tunashirikiana kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa, halmashauri, taasisi kama TANESCO na wadau wengine, hasa katika kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kitaifa, ikiwemo Mwenge wa Uhuru," ameeleza.
Kwa
ujumla, kiwanda cha Stalick kimejipambanua kuwa mdau muhimu wa maendeleo katika
Mkoa wa Pwani kwa kuwekeza si tu katika uzalishaji, bali pia katika ustawi wa
jamii kwa kupitia ajira, miradi ya kijamii na ushirikiano wa karibu na wadau wa
Sekta ya Madini na maendeleo ya jamii.

AKAGUZI wa Migodi ya Madini na Baruti wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, kuongeza ufanisi na kufuata taratibu na sheria za nchi katika utoaji wa huduma.
Hayo yamesemwa leo Mei 29, 2025 na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando jijini Mwanza wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha wakaguzi migodi na baruti ambacho kililenga kujengeana uwezo ikiwemo kufanya maboresho ya Kanuni mbalimbali za madini na Sheria ya Baruti.
‘’Tusikubali kuyumba au kuyumbishwa na hatimaye kutolewa kwenye mstari, tuendelee kufuata misingi, weledi na maadili katika utendaji kazi kwa kuepuka rushwa na kushinda vishawishi na tamaa nyinginezo,’’amesema Mhandisi Kamando na kuongeza,
“Nitoe rai, tunatakiwa kuwajibika kwa kuzingatia nidhamu, uaminifu, uwazi na kuongeza bidii kwenye kazi katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa,"amesema.
Aidha, Mhandisi Kamando amesema kuwa kikao hicho pia kimetoa mapendekezo ya maboresho ya Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira kwasababu zimepitwa na wakati kwa kuwa maboresho ya Sheria za Madini Sura ya 123 yalifanyika mwaka 2017 kwa mara ya kwanza na Kanuni husika hazijarekebishwa hadi hivi sasa.
“Kutokana na marekebisho ya Sheria ya Madini ni vyema sasa tukafanya maboresho ya kanuni za usalama, afya na mazingira ili ziweze kwenda sawa na Sheria na hivyo, kuimarisha ufanisi wa kazi, lakini pia kuna Sheria ya baruti ya mwaka 1963 na kanuni zake za mwaka 1964 nazo tumeona tufanyie maboresho ili usimamizi wa baruti nchini uwe mzuri zaidi,”amesema Mhandisi Kamando.
Naye Mwanasheria Mwandamizi wa Tume ya Madini, Damian Kaseko akiwasilisha mapendekezo ya Sheria ya Baruti, Sura ya 45 ambayo ilitungwa mwaka 1963 ameeleza kuwa maboresho yanayopendekezwa yanalenga kuboresha vifungu mbali mbali ili kuleta ufanisi katika usimamizi wa utekelezaji wa sheria husika.
Kwa upande wake Siri Boga, akizungumza kwa niaba ya washiriki amesema kikao kazi hicho kimewajengea uwezo wakaguzi wa madini huku wakipatiwa mbinu mpya ambazo wanapaswa kuzifuata wakati wa ukaguzi.
Wakati huo huo Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs), Maige Makolobela akizungumza amesema kikao hicho ni muhimu kwa wakaguzi kupata mafunzo ya pamoja, kubadilishana uzoefu na wenye migodi mikubwa.
“Tuna vijana wameingia Tume ya Madini bado hawajafahamu vitu vingi, hivyo ni fursa nzuri kwa vijana katika sekta yetu kujifunza kupitia vikao kazi kama hivi,”amesema.
Amesema, sheria ya baruti ni ya muda mrefu hivyo wamejaribu kuona ni namna gani wanaweza kuiboresha ukizingatia wakati inatungwa na hali ya sasa ni tofauti kutokana na ongezeko la migodi.
Naibu
Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya umeme katika Vitongoji kwa
kuzingatia vigezo vya ziada ikiwemo ukubwa wa vitongoji, ukubwa wa Jimbo pamoja
na mahitaji ya kiuchumi na kijamii.
Lengo la kuweka vigezo hivyo ni kuhakikisha kuwa kila jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na nishati ya umeme.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 29, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Simanjiro, Mhe. Christopher Olesendeka aliyeuliza kwamba Serikali imejipangaje kutekeleza miradi ya Vitongoji kulingana na jiografia ya Wilaya ya Simanjiro ambapo umbali kutoka Kitongoji kimoja hadi kingine ni zaidi ya kilometa kumi.
"Mheshimiwa Naibu Spika, tunatekeleza miradi hii ya Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada, tumeangalia ukubwa wa jimbo husika, ukubwa wa Vitongoji na mahitaji ya kiuchumi na kijamii katika jimbo husika. Niwahakikishie Wabunge mtaona utofauti katika miradi hii tunayoitekeleza hivi sasa." Amesema Kapinga
Akijibu swali la Mbunge wa Nyasa Mhe. Stella Manyanya aliyeuliza kuhusu kitongoji cha Songea Pori kilichopo katika Kijiji cha Lunyele na Kitongoji cha Nindi kilichopo Kijiji cha Konganywita kufikishiwa nishati ya umeme, Mhe. Kapinga amesema Vitongoji hivyo vimefanyiwa upembuzi yakinifu na kubainika vinahitaji njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kati kwa umbali wa kilometa tatu.
Amesema Serikali inatarajia kuvipelekea umeme vitongoji hivyo kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB) ambao utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2025/2026.
Kuhusiana na kasi ndogo ya Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme katika Jimbo la Nyasa Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imeshakutana na Mkandarasa na kumuagiza kuweka Wakandarasi wadogo (sub contractors) katika miradi yake anayotekeleza.
Akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Mhe. Aida Khenani aliyetaka kauli ya Serikali kuhusu kusuasua kwa Mkandarasi ambaye amepewa kazi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika, Mhe. Kapinga amesema katika utekelezaji wa miradi ya Vitongoji Serikali imehakikisha inawapata wakandarasi wenye weledi.
Kuhusu Wakandarasi ambao wanasuasua, Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi huo wa umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika.
Aidha, amemuagiza kuchukua hatua za ziada kwa Mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa haraka na kwa weledi.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatarajia kuendesha mafunzo kwa Mawakili wote wa Serikali kutoka kwenye Wizara, taasisi za Serikali, mashirika ya umma, Ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waliopo nchi nzima kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Mafunzo hayo yatafanyika kuanzia tarehe 02 Juni, 2025 hadi tarehe 04 Juni, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Dkt. Ally Possi, Wakili Mkuu wa Serikali kwa waandishi wa habari wakati akizungumza nao leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Dkt. Possi amewaeleza kuwa Kauli mbiu ya mafunzo hayo kwa mwaka huu ni: “Ubobezi wa Kisheria kwa Ajili ya Kesho: Teknolojia, Mikakati na Mizania Binafsi kwa Mawakili wa Serikali katika Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”.
Kauli mbiu hii inaakisi mafunzo yatakayotolewa kwa Mawakili wa Serikali kwa kuwa imezingatia nafasi na majukumu ya Mawakili wa Serikali na tasnia ya sheria kwa ujumla kama nguzo ya maendeleo ya taifa letu kama ilivyoainishwa kwenye moja ya nguzo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayohusu Uchumi Imara, Jumuishi na Shindani inayolenga nchi yetu kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2050.
Dkt. Possi ameongeza kuwa “Hatuna budi kutoa mafunzo ya kimkakati kwa Mawakili wa Serikali ili waendane na mabadiliko mbalimbali katika Sekta ya Sheria ili wanasheria wa Serikali waweze kuwa na utaalam ambao utaboresha uwezo wao wa kitaaluma kuendana na maendeleo ya sasa duniani,” amefafanua Dkt. Possi.
Mafunzo ya mwaka huu yatajikita kwenye mada mbalimbali zitakazogusa mbinu za kisasa na ujuzi wa mifumo ya kisheria utakaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watapata nafasi ya kipekee ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wabobezi wa ndani na nje ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo sheria, teknolojia, uongozi na masuala ya kitaifa na kimataifa.
Mawakili
watafundishwa mada mbalimbali zikiwemo:-
i. Uelewa wa namna bora ya kuendesha majadiliano ili kufikia suluhu nje ya vyombo vya sheria;
ii. Uelewa mpana wa sheria za uwekezaji;
iii. Uelewa wa fidia na madai ya uvunjaji wa mikataba;
iv. Sheria ya Masoko ya Mitaji Tanzania na nafasi ya Mamlaka na Baraza la Masoko la Mitaji katika utatuzi wa Migogoro; na
v. Usimamizi bora wa mikataba ya miradi ya ujenzi.
Vile vile Dkt. Possi amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, Mawakili wa Serikali watajifunza mbinu za kisasa zitakazowawezesha kufanya kazi kwa tija zaidi kwa kutumia teknolojia; watapata maarifa na uwezo wa ziada wa kutoa huduma za kisheria kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia mabadiliko ya kisheria na ya kijamii yanayoendelea kujitokeza.
Hivyo, Mawakili wa Serikali watakuwa na nafasi nzuri ya kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na kuitetea katika vyombo vya sheria kuendana na karne ya 21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Vilevile, Dkt. Possi amesema kuwa Ofisi yake imeendelea kuboresha na kuunda mifumo mbalimbali ya kieletroniki inayotumika kwa shughuli za Ofisi ili kuendana na mpango wa Taifa katika matumizi ya TEHAMA ambapo Ofisi itazindua Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa za Mashauri (Case Management Information System - CIMS) ambao unasajili mashauri yanayopokelewa na Ofisi, kuhifadhi taarifa mbalimbali za mashauri, takwimu na aina za mashauri yanayoendeshwa kwa kipindi husika. Pia, kutakuwa na uzinduzi wa tovuti na Maktaba Mtandao (Website & e-Library) na Mwongozo wa Chapa ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OSG Branding Manual).
Dkt.
Possi ametoa rai na kuwaalika Mawakili wa Serikali kushiriki mafunzo hayo
muhimu yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 mpaka 4 Juni, 2025 ambayo yatafunguliwa
rasmi na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza vipaumbele saba ambavyo itaavitekeleza katika Bajeti ya mwaka 2025/2026.
Vipaumbele hivyo vimetanagazwa Mei 29, 2025 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratoius Ndejembi wakati wa kusoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ardhi ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma.
“Maeneo ya kipaumbele yatakayotiliwa mkazo na Wizara katika mwaka 2025/26 ili kufikia malengo yaliyowekwa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na katika maeneo ya kimkakati’’ amesema Waziri Ndejembi.
Maeneo mengine ya kipaumbele ni kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma, ukusanyaji wa maduhuli na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kiutawala na kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.
Kwa mujibu wa Mhe. Ndejembi vipaumbele vingine ni kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii; kuimarisha mipaka ya kimataifa na kuendeleza miji ya mipakani, kuimarisha upatikanaji wa ramani ili kuwezesha uandaaji wa mipango mbalimbali ya kitaifa na matumizi mengine na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa vipaumbele.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba Shigeru ambaye amemuhakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano hayo.
Amekutana na kiongozi huyo leo (Alhamisi, Mei 29, 2025) katika ofisi ya Waziri Mkuu Tokyo, Japan, ambapo Mheshimiwa Majaliwa amesema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo kuwa pamoja na miradi mingine wanayotekeleza nchini, Japan kupitia JICA iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi ambayo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Amesema Waziri Mkuu wa Japan baada ya kupata maelezo hayo ameuelekeza uongozi wa JICA pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania Youichi Mikami kwenda kutembelea barabara hizo na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amepongeza kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kwamba ameahidi kuhakikisha makampuni mbalimbali ya Japan yataendelea kufanyakazi na Tanzania ili kuisaidia katika kukuza uchumi, kuendelea masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu nchini inaendelea kuongezeka.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amekutana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Japan Tobacco Inc (JTI) Masamichi Terabatake pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Mutsuo Iwai ambapo pamoja na mambo mengine ameishawishi ijenge kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la tumbaku mkoani Tabora.
Waziri Mkuu amesema kampuni hiyo ambayo ni miongoni mwa wanunuzi wakubwa wa tumbaku nchini na ndiyo inayoendesha kiwanda cha sigara kichopo Dar es Salaam kuwa ni vizuri wakapanua uwekezaji kwa kujenga kiwanda Tabora ili kurahisisha usafirishaji wa malighafi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku Barani Afrika na kwamba kampuni ya JTI inaongoza kwa kununua asilimia 25 ya tumbaku yote inayozalishwa nchini.
Naye, Rais na Mtendaji Mkuu wa Japan Tobacco Inc (JTI) Masamichi Terabatake ameahidi kuendelea kununua tumbaku nchini ambapo kwa mwaka huu wanatarajia kununua kilo milioni 33 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 190, ambapo mwaka 2024 walinunua kilo milioni 30 zilizokuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 165.
Pia amesema katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2026 hadi 2028 wanatarajia kutumia takribani Dola za Marekani milioni 1.5 kwa ajili ya kushirikiana na Serikali katika uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo afya, maji, elimu uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri Mkuu wa Japan Ishiba Shigeru kwenye mazungumzo rasmi yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uchumi kati ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tokyo nchini Japan, Mei 29, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)