Nafasi Ya Matangazo

March 22, 2025












Na Mwandishi Wtu, Mbeya
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka watumishi wa Tume ya Madini kuweka mikakati ya kuwainua wachimbaji wadogo wa madini kutoka kwenye uchimbaji mdogo wa madini na kuwa wa kati hatimaye kumiliki migodi mikubwa ya madini.

Mhandisi Samamba ametoa kauli hiyo mapema leo Machi 22, 2025 jijini Mbeya kwenye ufunguzi wa kikao cha kwanza cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Tume ya Madini lililoshirikisha wawakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Taifa na Mkoa, menejimenti ya Tume ya Madini na wawakilishi kutoka Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.

Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini kwa lengo la kuhakikisha wanapata soko la uhakika, kuwaunganisha na Taasisi za Kifedha kwa ajili ya kupata mikopo, elimu kuhusu njia salama za uchimbaji wa madini na kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kupitia kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content)

“Kiu ya Serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanaondoka kwenye uchimbaji mdogo wa madini na kuwa wa kati na wakubwa kwa kuwa watazalisha ajira zaidi kwa watanzania na kuongeza manunuzi ya ndani na Serikali kupata mapato yake kupitia kodi na tozo mbalimbali,” amesema Mhandisi Samamba.

Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa Tume ya Madini kubuni mifumo ambayo ni rafiki kwenye utoaji wa huduma yenye kuendana na teknolojia ya kisasa hasa kwenye ukusanyaji wa maduhuli na huduma za leseni za madini.

Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli katika Sekta ya Madini, Mhandisi Samamba amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini mafanikio makubwa yamepatikana kwenye ongezeko la maduhuli hali iliyopelekea Serikali kuongeza lengo la ukusanyaji wa maduhuli la kila mwaka.

“Kuongezewa lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa kila mwaka  ni ishara tosha kuwa Serikali ina imani kubwa na utendaji wa Tume ya Madini, na sisi kama Wizara ya Madini tutaendelea kuweka mazingira mazuri kwa watumishi wa Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na maboresho ya ofisi za Tume ya Madini Makao Makuu na za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, ununuzi wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari, mashine za upimaji wa madini ya metali kwenye masoko ya madini n.k,” amesisitiza Mhandisi Samamba.

Ameendelea kueleza kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua hadi kufikia asilimia tisa na kusisitiza kuwa lengo la asilimia 10 linatarajiwa kufikiwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Wakati huohuo,  Mhandisi Samamba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya Madini, ushirikiano na usimamizi makini wa Sekta ya Madini unaofanywa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Katibu Mkuu, Msafiri Mbibo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo sambamba na utendaji mzuri wa menejimenti ya Tume ya Madini na watumishi wote.

Awali akizungumza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema siri ya mafanikio ya utendaji wa Tume ya Madini ni pamoja na  ushirikiano mkubwa unaotolewa na Viongozi wa Wizara ya Madini ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kuanzia kipindi cha mwezi Julai hadi sasa Tume ya Madini imekusanya shilingi bilioni 750 ambayo ni sawa na asilimia 75 ya lengo lililowekwa na Serikali la kukusanya kiasi cha shilingi Trilioni Moja.

Amesema kuwa Tume ya Madini itaendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu katika kuhakikisha  watanzania wanaendelea kunufaika na rasilimali za madini.
Posted by MROKI On Saturday, March 22, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo