Moja ya changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa na Tanzania ikiwepo ni tatizo la ajira hasa kwa vijana. Nchini Tanzania, changamoto hii imekuwa ikiongezeka kutokana na mifumo ya elimu iliyokuwepo ambapo vijana walipokuwa wakihitimu ngazi mbalimbali za elimu kuanzia elimu ya msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu, walikuwa wakikosa ujuzi stahiki unaohitajika katika soko la ajira, na hivyo kubaki wakiwa hawana njia za kujiingizia kipato na kuendesha maisha yao. Hii ikapelekea ugumu wa maisha.
Kwa kutambua umuhimu wa stadi na ujuzi kwa vijana, serikali imekuja na mabadiliko ya mtaala wa elimu nchini ambapo sasa mwanafunzi atajifunza elimu ya mkondo wa kawaida pamoja na mkondo wa mafunzo ya amali (elimu ya ufundi), ili pindi atakapohitimu awe na uwanja mpana wa kuajiriwa au kujiajiri kutokana na kuwa na maarifa pamoja na ujuzi wa kutosha ambao ni muhimu sana katika ulimwengu wa sasa wa ushindani wa kazi, ajira na maendeleo.
Akizungumza na vyombo vya habari kabla ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema "Rais Samia alitangaza na kutoa maelezo akitaka Wizara ya Elimu ifanye kazi kubwa ya kupitia sera na lengo lilikuwa ni kuwa na sera ambayo itawaandaa wanafunzi kuwa mahiri katika kujibu mahitaji ya dunia ya sasa".
Aidha, Kwa kuzingatia umuhimu wa mabadiliko ya mtaala nchini, Februari 01, 2025, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Mabadiliko ya mtaala wa elimu na mafunzo umeambatana na mageuzi katika kufundishwa kwa somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Mafunzo ya ufundi stadi kuanzia elimu ya msingi na Matumizi ya akili unde (AI).
Lengo la mageuzi haya ni kuendana na mahitaji ya raslimaliwatu wenye tija yaani wenye ujuzi na ustadi yaliyopo kitaifa na kimataifa. Vilevile, ni kuwafanya wanafunzi na vijana kuwa mahiri na wenye maarifa, stadi, ujuzi na mitazamo chanya katika kuchagiza maendeleo ya taifa.
Katika uzinduzi huo, Rais Samia alisema " Ninachokiona mbele kinahitajika tuwe na maandalizi ya kutosha kwa kuzingatia ubora wa elimu yetu kwa kutoa elimu bora zaidi na kuandaa vizuri zaidi vijana wetu kumudu stadi muhimu zitakazowawezesha kuajiriwa na kujiajiri. Wataalamu wetu wamechambua vizuri mwenendo wa uchumi wetu, mwelekeo wa dunia, kasi ya maendeleo ya dunia na kujifunza kutoka kwa wenzetu, dhamira yetu ni kumwandaa kijana anayejiamini na mwenye nyenzo stahiki kukabiliana na ushindani na anufaike kiuchumi".
Kipekee, niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu chini ya uongozi wa Waziri mwenye dhamana Ridhiwani Kikwete kwa kuitafsiri vyema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023 na kufanyia kazi wajibu wa Wizara hiyo ya kuongeza fursa za ajira kwa vijana kuandaa mafunzo stadi kwa vijana 8,000 wenye umri kati ya miaka 15-35 katika fani mbalimbali huku serikali ikigharamia ada yote ya mafunzo kwa asilimia 100 huku wazazi na walezi wakigharimia mahitaji madogo madogo ya watoto wao.
Mafunzo yatakayotolewa yanahusisha fani za uashi, ufundi wa vyuma, useremala, ukataji wa madini, ubunifu wa mitindo na ushonaji, umeme wa majumbani. Fani nyingine ni ufundi bomba na magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, utengenezaji wa vipuli vya mitambo, upakaji rangi na maandishi ya alama, umeme wa majumbani na viwandani, huduma za hoteli na utalii.
Mafunzo haya yanatolewa katika vyuo mbalimbali vya ufundi vilivyopo katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini. Muda wa kuomba ni kuanzia Januari 30 hadi Februari 12, 2025. Niwasihi vijana kuchangamkia mafunzo haya ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata kipato kwa kuajiriwa na kujiajiri. Hii ni neema na fursa ambayo si ya kuichezea bali kuichangamkia ili kuharakisha maendeleo yao wenyewe na taifa lao pia.
Maoni: 0620 800 462.
0 comments:
Post a Comment