Tanzania imejaliwa kuwa na raslimali nyingi kama vile ardhi, bahari, vivutio vya utalii, madini, misitu kutaja kwa uchache. Raslimali hizi za asili zikiungana na raslimaliwatu, zikitumika vizuri, vinaweza kubadilisha maisha ya wananchi kutoka hali duni ya maisha (umaskini) kwenda kwenye hali nzuri (utajiri).
Umaskini ni moja ya changamoto kubwa kwa nchi za ulimwengu wa tatu ikiwemo Tanzania, ambapo juhudi mbalimbali zinafanyika kwa ushirikiano wa serikali, sekta binafsi, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi ili kupunguza tatizo hili.
Kwa Tanzania, sekta ya kilimo imechukua nafasi kubwa katika kutoa ajira ambapo zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo. Watanzania hawa ambao asilimia kubwa wanaishi vijijini, wanakidhi mahitaji yao kupitia kilimo kwa kupata chakula huku wakiuza mazao yao kwa ajili ya mahitaji mengine kama vile kujenga nyumba, kusomesha watoto na kununua vyombo vya usafiri kama vile pikipiki.
Kwa asilimia kubwa kilimo hapa nchini kinafanyika kwenye ardhi, lakini habari njema ni kwamba wananchi waishio pembezoni mwa bahari, mito na maziwa wanaweza kujishughukisha na kilimo cha zao la Mwani. Zao la Mwani huota na kukua kwenye maji chumvi na yasiyo chumvi. Hivyo basi wakazi waishio pembezoni mwa vyanzo hivyo vya maji, wanaweza kujishughukisha na kilimo cha Mwani, achilia mbali shughuli za uvuvi ambazo ndizo hufanywa na wengi.
WANANCHI TANGA MJINI WAONYESHWA FURSA KWENYE KILIMO CHA MWANI.
Wilaya ya Tanga ambayo ndiyo Makao Makuu ya mkoa wa Tanga ina raslimali nyingi, mojawapo kubwa ni uwepo wa bahari ambayo ndipo ilipo Bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga ndiyo moyo wa uchumi wa mkoa wa Tanga.
Katika harakati za kuwawezesha wananchi wa wilaya ya Tanga kujikwamua kiuchumi katika eneo la kilimo, Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu anawauma sikio wananchi kujikita kwenye kilimo cha Mwani ambacho ni kinastawi vyema baharini kwa kuzingatia kuwa wilaya ya Tanga haina maeneo makubwa ya kilimo kama zilivyo wilaya nyingine za Mkoa wa Tanga kama Lushoto, Korogwe, Pangani, Muheza, Mkinga, Kilindi na Handeni.
Kwa kuanzia, Ummy ameanza na wakulima 200 ambao ametafuta ufadhili kutoka taasisi isiyo ya kiserikani ya Korea iitwayo Good Neighbours Foundation ili kuwajengea uwezo wakulima wa wilaya ya Tanga Ili waweze kulima kisasa zao la Mwani ili kujikomboa kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Katika msisitizo wake, Ummy Mwalimu anasema "Bahari ndiyo shamba na mgodi wa wananchi wa Tanga Mjini, hivyo basi, wananchi watumie fursa ya uwepo wa bahari si tu kwa shughuli za uvuvi lakini pia kwa shughuli za kilimo cha zao la Mwani."
Oktoba 2024, Jijini Tanga, yalifanyika mafunzo awamu ya kwanza ya siku nne kwa wakulima 50 wa zao la Mwani kutoka maeneo ya Mundura, Mwarongo, Saadani, Kiwavu, Kivindani na Machui.
Mafunzo haya yaliambatana na kujengewa uwezo wa kulima kisasa zao la Mwani, aina za Mwani, utunzaji na uhifadhi, masoko na faida za Mwani kiuchumi na kiafya. Katika mafunzo hayo, wakulima 100 walipatiwa kamba ambazo ni nyenzo muhimu katika kilimo hiki.
Novemba 11, 2024, Jijini Tanga, yalifanyika mafunzo ya awamu ya pili ya siku nne kwa wakulima wengine 50 wa zao la Mwani kutoka kata tano za Tongoni, Mnyanjani, Tangasisi, Mzingani na Masiwani ili kuwa na uelewa mpana, hatimaye zao hili liweze kubadili maisha ya wananchi hao.
Katika mafunzo hayo, Ummy Mwalimu alisema " Tunataka mlime Mwani kisasa, lakini si tu mlime lakini pia mpate faida kwa sababu mwisho wa siku tunataka mpate pesa za kujenga nyumba, kusomesha watoto na kufanya shughuli nyingine za maendeleo".
Kwa hakika, wananchi wa Tanga Mjini wanaweza kubadili maisha yao kupitia uwepo wa bahari kwa kulima zao la Mwani. Uwepo wa Bahari Tanga ni neema, ni mgodi zaidi ya mgodi wa dhahabu na ndiyo maana Ummy Mwalimu anasema " Bahari yetu, mgodi wetu, Mwani wetu, dhahabu yetu.
0 comments:
Post a Comment