Nafasi Ya Matangazo

December 21, 2024








Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itendelea kubuni mikakati ya kuimarisha sekta ya Maliasili na Utalii kwa kuwa sekta hiyo ni nguzo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
 
Amesema hayo jana (Ijumaa, Desemba 20, 2024) wakati alipozindua Tuzo za Uhifadhi na Utalii katika Ukumbi wa Hoteli ya Mt. Meru jijini Arusha. Tuzo hizo zinalengo la kuchochea ushindani kati ya wadau wa sekta ya maliasili na utalii nchini.
 
Amesema kuwa Sekta ya maliasili na utalii ni chanzo kikubwa cha mapato ya Taifa kwa kuwa inahusisha shughuli nyingi za kiuchumi. “Sekta hii peke yake inachangia asilimia 21.5 katika pato ghafi la Taifa ambapo asilimia 17.2 ni utalii, asilimia 4.3 ni misitu na nyuki”.
 
Aidha, amesema kuwa Sekta hiyo inachangia asilimia 30.9 ya mapato ya fedha za kigeni ambapo asilimia 25 yanatokana na utalii na asilimia 5.9 ni misitu na nyuki.
 
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa juhudi za dhati na maono makubwa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuiendeleza Sekta ya Maliasili na Utalii yamesaidia kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023.
 
“Jitihada za Rais wetu Dkt. Samia zimesaidia pia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na Utalii wa Kimataifa kwa asilimia 68.2 kutoka dola za Marekani bilioni 2.0 mwaka 2021 hadi bilioni 3.4 mwaka 2023”
 
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha  inaweka vigezo vya wazi na vinavyojulikana vya uteuzi na upokeaji wa tuzo. “Vigezo hivyo, pamoja na mambo mengine viwe vinavyozingatia ubora katika uhifadhi wa mazingira, huduma za utalii, usimamizi wa hifadhi za Wanyama na uendelezaji wa maeneo ya utalii”
 
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amempongeza Rais Dkt. Samia kwa namna mnavyojitoa katika kuhakikisha Sekta ya Maliasili na Utalii inaendelea kukuwa kwa kasi.
Posted by MROKI On Saturday, December 21, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo