Nafasi Ya Matangazo

November 09, 2024

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,  Dkt.James Mataragio (tatu kulia) akiongoza kikao kati ya  Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,  Dkt.James Mataragio (tatu kulia) akiongoza kikao kati ya  Wizara na Kampuni ya Equinor Tanzania AS. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.
Makamu wa Rais wa Equinor Kanda ya Bara la Afrika, Bi. Nina Birgitte ( wa Pili kshoto) akizungumza wakati wa kikao kati ya kampuni hiyo na  Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika.
************
Wizara ya Nishati imekutana na kufanya mazungumzo na Kampuni ya Equinor Tanzania AS kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) pamoja na masuala mengine yanayohusu Gesi Asilia nchini.

Mazungumzo hayo yalifanyika hivi karibuni Jijini Cape Town – Afrika Kusini wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika, mkutano ulioleta pamoja wadau zaidi ya 5000 kutoka ndani na nje ya Afrika.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alisema kuwa Wizara ipo tayari kusikiliza na kuchukua mapendekezo yatakayotolewa na kampuni hiyo yanayolenga kuwezesha utekelezaji wa mradi kwa wakati.

“Niishukuru Equinor Tanzania kwa kuomba kikao hiki muhimu na Wizara. Tunatambua kuwa utekelezaji wa mradi huo wa kusindika gesi asilia  unahusisha wadau wengine ambao hawapo hapa ila hiyo haizuii Wizara kukutana na kumsikiliza mdau mmoja mmoja kwani lengo letu ni kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi.” alisema Mataragio.

Ujumbe wa Equinor uliongozwa na Makamu wa Rais wa Equinor Kanda ya Bara la Afrika, Bi. Nina Birgitte ambaye  pamoja na kueleza masuala ya LNG na kutoa ushauri kwa Wizara,  alitumia fursa hiyo  kutoa taarifa ya mabadiliko ya uongozi wa juu wa kampuni hiyo nchini Tanzania ambapo alisema nafasi ya Maneja wa Equinor Tanzania ambayo kwa sasa inashikiliwa na Dr. Unni Fjaer itachukuliwa na Bi. Hilde Nafstad kutoka Norway.

Kampuni ya Equinor Tanzania AS ni miongoni mwa wabia wanaohusika katika utekelezaji wa mradi wa LNG nchini Tanzania.

Mradi huo unaolenga kuendeleza gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha Bahari ya Hindi Kusini mwa Tanzania, unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani takribani Bilioni 42.

Viongozi wengine kutoka Tanzania waliohudhuria kikao hicho ni Kamishna Msaidizi wa Petroli, Mha. Joyce Kisamo,  Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Bw. Mussa Makame.
Posted by MROKI On Saturday, November 09, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo