Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara ya Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff leo tarehe 19 Novemba, 2024 amekutana na kufanya kikao na Mameneja wa Mikoa kwenye Ofisi za Makao Makuu za Wakala hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Katika kikao hicho Mhandisi Seff amewataka Mameneja hao kwenda kuwasimamia Mameneja wa Wilaya katika maeneo yao na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Amesema Mameneja hao wanapaswa kulinda taaluma zao pale wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ili kulinda sifa nzuri ya Wakala.
Aidha, Mhandisi Seff amewataka Mameneja hao kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye miradi wanayoitekeleza katika Wilaya zao.
“Nimepita kwenye baadhi ya Mikoa na Wilaya,nimeona kuna barabara ambazo hazifanyiwi matengenezo. Pia yapo madaraja ambayo hayasafishwi na hivyo kuweza kuleta madhara wakati wa msimu wa mvua”.
Hivyo amewataka Mameneja hao kwenda kusimamia na kuhakikisha wanafanya matengenezo ya barabara kama inavyotakiwa pia kusafisha madaraja ili kutokuleta mafuriko wakati wa msimu wa mvua unaokaribia.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Azimina Mbilinyi amewataka Mameneja hao kuwasimamia vyema watumishi walio chini yao kwenye utunzaji wa vifaa vya kazi, utunzaji wa siri pamoja na kushirikiana na taasisi nyingine zinazowazunguka kwenye Mikoa yao.
0 comments:
Post a Comment