Nafasi Ya Matangazo

October 11, 2024

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani kwa mwaka 2024, yaliyofanyika katika mji mdogo wa Ushirombo, Wilayani Bukombe mkoani Geita, Octoba 11, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haijatoa maagizo ya kuwaondoa kazini walimu wa cheti bali amewataka watumie mpango wa mafunzo endelevu kazini kwenda vyuoni kusoma.

Amesema Serikali imefanya maboresho ya sera na mitaala ya elimu nchini ambayo pamoja na mambo mengine imeleta mabadiliko katika sifa za chini za mwalimu katika shule za msingi kuwa Stashahada/Diploma. “Pamoja na mabadiliko haya, Serikali inatambua kuwa bado wapo walimu ambao hawajafikia sifa ya kuwa na Astashahada au Diploma na hakuna agizo la kuwataka waondolewe katika ajira,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Oktoba 11, 2024) wakati akizungumza na mamia ya walimu na wadau walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa mpira wa shule ya sekondari Ushirombo, wilayani Bukombe, mkoani Geita.

Amesema walimu wote ambao hawana sifa ya Astashahada au Diploma watumie fursa ya mpango wa mafunzo endelevu kazini kwenda vyuoni kusoma ili kupata sifa ya diploma au kujiendeleza kupitia moduli kwa mfumo wa LMs - Learning Management System chini ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE). 

“Kupitia mfumo huu, Serikali imeingia makubaliano na kampuni ya simu ya Airtel kwa walimu wenye vishikwambi na wanatumia mtandao wa Airtel kupakua moduli bure kwa ajili ya kujiendeleza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, taasisi za elimu, sekta binafsi na wadau wa sekta ya elimu nchini wahakikishe walimu wanajengewa mazingira bora ya kazi ili watimize majukumu yao kwa ufanisi.

Aidha, amewataka waimarishe programu za mafunzo kwa walimu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia huku akiwataka waajiri kuwapa mafunzo walimu pamoja na taasisi zinazohusika na udhibiti wa ubora waendelee kutimiza majukumu yao.

Katika kuboresha sekta ya elimu nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha na kusimamia miundo ya watumishi wakiwemo walimu. “Serikali imeboresha stahiki za msingi za watumishi kwa kupandisha madaraja na kuhakikisha wanapata nyongeza ya mishahara yao kwa wakati.” 

Akianisha maboresho mengine, Waziri Mkuu amesema: “Serikali imeimarisha miundombinu mahali pa kufanyia kazi ikiwemo kuhakikisha kuna madarasa, maabara, mabweni, majengo ya utawala na sasa tumeingia kwenye ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na kuimarisha ajira zao.”

Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Mradi wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), Mradi wa Huduma za Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira  (SWASH), Programu ya Uboreshaji Kada ya Ualimu (GPE - TSP) na Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo (EP4R).

Akielezea kuhusu upandishaji madaraja kwa walimu, amesema: “Kati ya Machi, 2021 na Agosti, 2024, walimu 601,698 nchi nzima wamepandishwa madaraja na Serikali imetumia shilingi trilioni 1.3 kuwalipa. Na niwatake Maafisa Elimu kuwatembelea walimu vijijini na kusikiliza kero zao,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi sasa, Serikali imeweza kuwabadilisha kada/miundo jumla ya watumishi 36,768 kwa gharama ya sh. 3,090,476,931.00 na imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 144,356 yenye jumla ya sh. milioni 229.9.

Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewashukuru walimu wa Tanzania kwa kuendelea kuiheshimisha taaluma yao na kuwa chanzo cha maarifa kwao hakitoki kwingine isipokuwa kwao hivyo wailinde kwa wivu mkubwa taaluma hiyo.

Dkt. Biteko amesema mwaka 2015 wakati anachaguliwa kuwa Mbunge, wilaya yake ilikuwa ikishika nafasi ya mwisho katika mitihani ya Taifa. “Nilizungumza na walimu kuhusu matokeo mabaya na wakasema tusiwaache walimu nyuma hivyo tulianza kukutana na kufanya tathimini na sasa tunafanya vizuri.”

Amesema viwango vya ufaulu vimekuwa vikiongezeka kila mwaka huku akitolea mfano wa matokeo ya mwaka jana kwamba darasa la saba wilaya hiyo ilishika nafasi ya pili katika mkoa huo, darasa la nne ilipata wastani wa asilimia 78 na kuwa nafasi ya pili kimkoa.

“Kidato cha pili tulikuwa na ufaulu wa asilimia 98, kidato cha nne ufaulu ulikuwa asilimia 96, kidato cha sita ulikuwa asilimia100 na hizi zote tulikuwa wa kwanza. Katika mitihani ya mock ya kanda ambayo ilijumuisha mikoa mitano yenye Halmashauri 37, Wilaya ya Bukombe tumeshika nafasi ya tatu, tukiwa nyuma ya Ilemela na Nyamagana. Hivyo, niliona tutenge siku moja ya kusema asante mwalimu.”

Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa walimu nchini wasivunjike mioyo waendelee kufanya kazi yao na kuwa maisha yao ni kielelezo cha mafanikio katika Taifa na kuwa wao ni nyota inayoangaza na yeye ataendelea kushirikiana nao.

Mapema, Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania, Mkoa wa Geita, Pauline Tinda alisema kuwa tangu mwaka 2019, Wilaya Bukombe imekuwa ikiadhimisha Siku ya Mwalimu ambayo inalenga kuteleza maelekezo ya ILO na UNESCO ya kuwatambua na kutoa tuzo za umahiri kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha masomo ya kusoma, kuandika na kuhesabu.

Aidha ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi kwa walimu ma ustawi wa walimu kwa kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuwapandisha madaraja. Pia alimshukuru Dkt. Biteko kwa kuendelea kuthamini mchango wao katika jamii.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kuwa benki hiyo inatambua umuhimu wa walimu nchini na kuwa watu wengi wamefanikiwa kutokana na mchango wao.

“Sisi tunawapongeza walimu wote nchini. Tumeendelea kuunga jitihada nzuri zinazofanywa ili mwalimu awe na mazingira mazuri ya kufanya kazi. Hadi sasa tumetoa zaidi ya shilingi bilioni moja ili kununua madawati na leo tunachangia madawati 545 na magodoro 88 kwa shule mbalimbali za wilaya hii ili kusaidia elimu ya Tanzania iwe bora zaidi,” alisema.



Posted by MROKI On Friday, October 11, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo