RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatika nchini kupitia sekta ya utalii yanayoitangaza Tanzania kimataifa na kuitambulisha duniani kuwa nchi ya kwanza Afrika inayofanya vizuri kwa utalii na ya sita dunia nzima.
Amesema mafanikio hayo ni juhudi zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha miundombinu ya utalii ikiwemo kuendelea kuliimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL),
Pamoja na kuhamasisha mashirika mengine ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na nchi zenye masoko ya utalii, kujenga barabara na reli za kisasa zinazounganisha vivutio vya utalii, kujenga na kukarabati viwanja vya ndege, na kuimarisha huduma nyengine muhimu za utalii.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo, ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es salaam kwenye hafla ya ufunguzi wa Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Swahili (8th edition of the swahili international tourism expo – site 2024).
Amesema kutokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan za kukuza utalii nchini, Tanzania imeshuhudia idadi kubwa ya watalii wa kimataifa wanaotembelea sehemu mbalimbali za nchi pamoja na ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii.
Ameeleza pamoja na hatua hizo, Serikali pia imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji kwenye Sekta ya Utalii hususan eneo la huduma za malazi.
Aidha Dk. Mwinyi ameeleza kwa mujibu wa takwimu kutoka sekta ya utalii, hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 zinaonesha kuwa Tanzania imepokea idadi ya watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kuwahi kufikiwa katika historia ya Tanzania na mapato yatokanayo na sekta hiyo, kufikia Dola za Marekani bilioni 3.5.
Amebainisha kuwa, sekta ya utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania, huku ikichangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa, asilimia 25 ya mauzo ya nje na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa mafanikio hayo yameitambulisha Tanzania kimataifa kuwa ni nchi ya sita duniani na ya kwanza Afrika kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwezi Septemba, 2024 na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism – World Tourism Barometer).
Mafanikio mengine ya Utalii kwa Tanzania, Dk. Mwinyi alieleza kuwa ni tuzo mbalimbali za kimataifa zilizopokelewa nchini zikiashiria ubora na upekee wa vivutio vilivyomo mbali na huduma zitolewazo na sekta ya utalii, zikiwemo tuzo za mwaka 2023 za “World Travel Awards (WTA)” ambao waliitambua Bodi ya Utalii Tanzania kama “Africa’s Leading Tourist Board,” Kisiwa cha Thanda Shunghumbili, Mafia kama “World Leading Exclusive Private Island”, Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kama “Africa’s Leading Tourist Attraction,” na Hifadhi ya Taifa Serengeti kama “Africa’s Leading National Park”.
Pia, mtandao wa “Trip Advisor” umezitambua Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire kama “Africa’s Top Attractions” mwaka jana Pamoja na “Island Index” wameitaja Zanzibar kuwa “The 2nd Best Island Destination in the World” kwa mwaka 2024.
Dk. Mwinyi amesema kuwa utalii ni sekta yenye ushindani mkubwa kimataifa, bila kuweka nguvu kubwa kwenye utangazaji, haiwezi kufikia malengo yaliyojiwekwa.
Hivyo, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Bodi ya Utalii Tanzania, kwa kazi nzuri wanayoifanya kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi pamoja na maandalizi mazuri ya Onesho la “SITE 2024” kwa kiwango cha kimataifa limechangia ushiriki wa wadau wakubwa wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi hali aliyoisifu imeongeza kasi ya kuitangaza nchi kimataifa kupitia Utalii kwa kufungua fursa za biashara kati ya wafanyabiashara wa ndani na masoko ya nje ya utalii.
0 comments:
Post a Comment