Timu shiriki kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), zimeonesha nidhamu bora ndani na nje ya uwanja, imeelezwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya michezo ya SHIMIWI 2024, Apollo Kayungi iliyoanza tarehe 18 Septemba, 2024 mkoani Morogoro, ambapo amesema hakuna hali ya utovu wa nidhamu iliyoripotiwa na waamuzi viwanjani na hata kwenye kambi ambazo timu zimefikia.
“Napenda kuwapongeza viongozi na wachezaji kwa kuonesha nidhamu nzuri wanayoonyesha michezoni inaleta taswira nzuri hata wananchi wanapokuja kuangalia michezo wanaona, imedhihirisha timu za watumishi wa umma na timu nyingine,”amesema Kayungi.
Halikadhalika amesema michezo inakwenda salama, ambapo sasa tarehe 27 Septemba, 2024 wanatarajia kuingia kwenye hatua ya 16 bora kwa michezo ya kuvutana kwa kamba, mpira wa netiboli na miguu, ambazo zilicheza hatua ya makundi yaliyokuwa nane kwa kila mchezo.
Timu zilizoshiriki ni 68 kati ya hizo zinazocheza mpira wa miguui ni 41 na zinazobaki ni netiboli, michezo ya jadi na mbio za baiskeli.
Ametoa wito kwa kuwaomba waajiri kutekeleza agizo la mlezi wa SHIMIWI, Katibu Mkuu Kiongozi kwa kutenga bajeti kwa ajili ya watumishi kushiriki kwenye michezo mbalimbali, ambayo inawasaidia kulinda afya zao.
Katika mchezo wa mpira wa miguu timu ya TAKUKURU wamewafunga Wizara ya Kilimo kwa magoli 4-0; Wizara ya Maendeleo ya Jamii wametoka sare na Wizara ya Ulinzi kwa bao 1-1; RAS Katavi wamewafunga Wizara ya Viwanda na Biashara magoli 2-0; Wizara ya Katiba na Sheria waliwafunga Tume ya Utumishi kwa magoli 3-2; Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo waliwashinda Ofisi ya Waziri Mkuu Sera 2-1 na RAS Simiyu waliwafunga ndugu zao RAS Singida kwa magoli 1-0; nazo timu za Ofisi ya Ukaguzi waliwafunga TARURA kwa bao 1-0; na Hazina waliwashinda RAS Tanga kwa 3-0.
Katika mchezo wa kuvutana kwa kamba kwa wanawake timu ya Uchukuzi wamewavuta Bodi ya Pamba kwa 2-0; nao Wizara ya Maji wametoka sare na Wizara ya Maji kwa 1-1.
Kwa upande wa mchezo wa netiboli timu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii waliwashinda RAS Dar kwa magoli 28-13; nao Wizara ya Maji waliwafunga TAMISEMI kwa 20-19; Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo walifungwa na Wizar aya Afya kwa magoli 48-11; huku Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) waliwafunga Mashtaka kwa 23-20.
Michezo mingine Wizara ya Ardhi wamewafunga RAS Singida kwa magoli 29-20; timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wamewachapa RAS Dodoma kwa 44-9; Wizara ya Mifugo wamewaliza Mambo ya Ndani kwa 21-7; Wizara ya mambo ya Nje waliifunga Ofisi ya Maadili ya Viongozi kwa magoli 35-29; Mahakama waliwafunga RAS Lindi kwa magoli 41-10.
0 comments:
Post a Comment