MWENYEKITI wa ACT-Wazalendo Taifa Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ni wakati sasa vijana kujitambua na kusimama imara katika kuitetea Nchi na kupigania haki zao.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Leo Jumamosi Septemba 28, 2024 aliposhiriki, akiwa Mgeni Rasmi, katika Hafla ya Ufunguzi wa Kongamano la Vijana wa ACT-Wazalendo, wa Mkoa wa Kichama wa Micheweni, huko katika Ukumbi wa Chama hicho 'Kwa Sadam' uliopo Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema msimamo thabiti wa vijana, ni silaha muhimu ya kutetea haki zao, pamoja na ni nguvu ya pekee katika kupigania maslahi na Mamlaka Kamili ya Zanzibar.
Mheshimiwa Othman amefahamisha akisema, "utu na heshima ya vijana pamoja na ya Nchi hii ni muhimu na ni kipao mbele zaidi kwa sasa, hivyo vijana ni lazima kujitambua, kujitathmini, na msikubali kudanganywa kwa kulinda maslahi ya watawala wachache ambao hawana uchungu na maendeleo yenu".
Amesema ni kauli zisizo na ukweli asilani za watawala kusema wataleta maendeleo nchini huku chama chao kikitawala kwa miaka yote, "iwapo wanaahidi kuleta maendeleo sasa kwani hapo kabla walishindwa nini ilhali wao ndio walikuwa watawala wa nchi hii tangu kuasisiwa tena mfumo wa vyama vingi ".
Aidha amewahimiza vijana wa chama hicho kujifunza na kupambana kwa hoja kwani dunia ya sasa inahitaji mbinu na hoja uhakika 'facts' na siyo maneno ya mchele.
Mheshimiwa Othman amewaeleza vijana kwamba Viongozi Wakuu wa Chama hicho wamechukua ahadi ya kuongoza mapambano bila kuchoka katika kupigania maslahi na haki ya vijana na Wazanzibari wote.
Katika Salamu zao, zilizotolewa na Viongozi wao wa Kitaifa, Makamu Mwenyekiti, na Katibu wa Ngome Taifa Ndugu Nassor Marhun na Mohamed Busara, wameeleza kuwa Ngome ya hiyo ipo imara, Micheweni na katika Tanzania yote, na kwamba sasa wapo tayari kuulinda ushindi wa kura zao ifikapo Oktoba 2025, ili kuhakikisha Zanzibar inajikwamua na kupata Mamlaka yake Kamili.
Akitoa salamu za Vijana wa Mkoa wa Kichama wa Micheweni, Mwenyekiti wao, Bi Moza Masoud Ali, amesema "lipo kundi la Vijana kutoka Vyama vyengine, kikiwemo Chama Tawala, ndani ya
Mkoa huu, ambao wameishiwa na wamedanganyika, sasa hupachika Bendera za ACT- Wazalendo na huvaa Sare za Chama chetu, baadae huzishusha wakidai wamekihama Chama".
"Tunawahakikishia Viongozi wetu Wakuu kwamba Micheweni tupo imara na tayari kuipambania Nchi hii", amesema
Kongamano hilo lililobeba Anuani ya 'Mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu hali bado ni tete, nini wajibu wa Vijana?, lililoanza kwa Matembezi ya Amani limewajumuisha Viongozi wa Ngazi mbali mbali katika ACT-Wazalendo, kutoka Tanzania Bara na Zanzibar; wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti na Naibu Katibu Mkuu ACT- Wazalendo Zanzibar Ndugu Ismail Jussa, na Omar Ali Shehe: pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Vijana Taifa Ndugu Rukaiya Nassir.
Hafla hiyo imeambatana na harakati mbali mbali za Burudani, zikiwemo Utenzi na Wimbo Maalum wa Chama.
Mheshimiwa Othman yupo Kisiwani Pemba, kwaajili ya Ziara Maalum inayojumuisha shughuli za Chama na Serikali.
Katika Ziara hiyo, Mheshimiwa Othman ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib.
0 comments:
Post a Comment