Nafasi Ya Matangazo

September 27, 2024


Na; Mwandishi Wetu - Sengerema
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amekabidhi vifaa mtaji kwa vikundi vya Vijana na Watu wenye Ulemavu vyenye  thamani ya zaidi ya shilingi milioni 90 kwa vikundi 16 vya vijana wa wilaya ya Sengerema.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo leo Septemba 27, 2024, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa  vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja na vifaa vya kushonea (cherehani),Mashine ya kutotolesha vifaranga,Kompuyta na Printer, Mitungi ya gesi, Majiko na Majokofu na Mashine ya Kusaga.

Aidha, Waziri Ridhiwani amesema Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu na kusimamia afua mbalimbali za kuwezesha vijana nchini katika maeneo ya kiuchumi na kijamii ili vijana waweze kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na stadi zitakazowawezesha kufanya shughuli zitakazo waingizia kipato na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango wa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa na rasilimali watu muhimu katika kukuza uchumi wa nchi,” amesema 

Kwa upande mwengine, Mhe. Ridhiwani ametoa rai kwa vijana wote nchini kuhakikisha kuwa wanaendelea kutekeleza wajibu wao kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwezeshaji kiuchumi ili kujipatia ajira na kuweza kujitegemea.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Mhe. Senye Ngaga amemuhakikishia mheshimiwa Waziri kuwa Wilaya hiyo imejipanga kuendelea kuwezesha vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye Ulemavu.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Sengerema, Mhe. Hamis Tabasamu, ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za miradi ikiwemo miradi ya elimu, barabara, umeme, sekta ya afya na maji safi. Sambamba na hayo ameipongeza serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwezesha vijana wa wilaya hiyo kujiajiri na kuajiri vijana wenzao. 

Mwakilishi wa vikundi vya vijana vilivyonufaika, Clement Cosmas ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vitaenda kuwasaidia kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.








Posted by MROKI On Friday, September 27, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo