Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga leo Septemba 22, 2024 imeandika historia mpya kwa kuzindua rasmi tamasha lake la kwanza la Utalii linalolenga kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Akizungumza muda mfupi kabla ya uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia Utalii), Nkoba Mabula, alisisitiza umuhimu wa tamasha hili katika mkakati wa kuimarisha utalii.
"Tamasha hili lililobeba kauli mbiu "ALIANZISHA MAMA SISI TUNAENDELEZA" ni sehemu ya juhudi za kukuza utalii, kuvutia wawekezaji, na kutoa huduma bora kwa watalii," anasema.
Mabula alieleza kuwa lengo ni kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni tano na mapato ya utalii kufikia dola za Marekani bilioni sita.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa kila mmoja ni muhimu ili kufanikisha malengo hayo, hasa katika kutoa huduma bora kwa watalii ili kuwahamasisha kurudi tena lakini pia kuboresha miundombinu ili kuendeleza uhifadhi.
Aidha kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Pindi Chana, Mabula aliipongeza mkoa wa Tanga kwa kuandaa matamasha ya mara kwa mara, akibainisha kuwa hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
"Matamasha kama haya yana mchango mkubwa katika kufikia malengo ya kukuza utalii na ni mfano wa kuigwa na mikoa mingine, kwa niaba ya wizara, niendelee kutoa rai kwa viongozi wenzangu tuendelee kutumia matukio mbalimbali wananchi kutembelea vivutio vya utalii ili kukuza utalii wa ndani" alisisitiza.
Mabula pia alihitimisha kwa kuwataka viongozi na wadau mbalimbali wanaotoa huduma katika mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora ili watalii wanotembelea vivutio hivyo washawishike kurudi na kuvitangaza kwa ndugu na jamaa zao.
Aliongeza kuwa, Mhe. Rais alielekeza wadau wote wa utalii kushirikiana ili kuyaendeleza matukio ya namna hiyo katika kutangaza utalii na biashara na hivyo kutoa rai kwa mikoa na halamashauri nchini kuendelea kushirikiana na wadau wa utalii katika kubuni matukio ya utangazaji wa utalii, na kusisitiza Wizara yake kutoa ushirikiano wakutosha.
“Kupitia Mhe. Rais sasa hivi ipo fedha imetengwa mahususi kwaajili ya kuendeleza sekta ya utalii katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya mikoa na wilaya, ni juhudi yetu sisi kuhakikisha kwamba vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yetu vinatambulika na Wizara, ivione na viweze kuelezeka kwa ufasaha kwaajili ya kuvitangaza,” anasema.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, alielezea umuhimu wa utalii katika uchumi wa Tanzania, akisisitiza kuwa tamasha hilo linatoa fursa ya kipekee ya kuonyesha vivutio vya utalii vya Mkoa wa Tanga, kama vile Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Milima ya Usambara.
Aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa maandalizi mazuri na kutoa rai kwa Halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
Dkt. Burian pia aliwasihi wananchi kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani ili kusaidia kukuza uchumi wa taifa. “Kutembelea vivutio vyetu ni hatua muhimu ya kukuza utalii wa ndani na kuimarisha uchumi wa taifa,” alisema, akibainisha kuwa idadi ya watalii inaongezeka kila mwaka na mwaka huu pekee inatarajiwa kufikia zaidi ya watalii 105,230.
Katika hafla hiyo, Dkt. Burian alizindua Jengo la Utalii (Tourism Information Center) pamoja na Mpango Kazi wa Utalii, huku akiwahimiza wadau wote kutoa taarifa sahihi kuhusu vivutio vya utalii ili kuvutia wageni zaidi.
Tamasha la Utalii Lushoto, ambalo linaonesha utamaduni, michezo, na burudani mbalimbali, linatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii na uchumi wa Mkoa wa Tanga. Aidha, tamasha hili linalenga kutoa fursa kwa wageni wa ndani na nje kuona vivutio vya utalii vya Lushoto na kuhamasisha wananchi kuendelea kuwekeza katika sekta hii muhimu.
0 comments:
Post a Comment