Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe Mhe. George Simbachawene akiongea na wananchi wa Chipogolo kwenye mkutano wa hadhara uliolenga kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
*******************
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge
wa Jimbo la Kibakwe Mhe. George Simbachawene ameelekeza viongozi wa maji katika
kata ya Chipogolo Jimbo la Kibakwe kuuza maji kwa shilingi elfu moja mia mbili
tu ili wananchi wengi waweze kumudu gharama na kuyatumia maji ipasavyo.Maelekezo hayo yametolewa na Mhe. Simbachawene wakati alipokuwa akiongea na wananchi wa Chipogolo kwenye mkutano wa hadhara uliolenga kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
“Nimesikia kilio chenu kuhusu gharama kubwa za maji na inaonekana ni kero kubwa.
Sasa
niwahakikishie kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda sana na
hataki kusikia wananchi wake wanapata shida ya huduma yoyote. Hivyo, ninawaelekeza
viongozi wanaosimamia huduma ya maji hapa Chipogolo kuacha kuwatoza wananchi kiasi
cha shilingi elfu mbili kwa unit isipokuwa kuanzia kesho tarehe 3 Agosti, 2024 itakuwa ni Shilingi elfu
moja na mia mbili tu” alisema Mhe. Simbachawene.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewaomba wananchi wa Chipogolo kufumbua macho, kutazama na kushukuru kwa maendeleo ambayo yameletwa na Rais Dkt. Samia kwa kuwa barabara sasa ni nzuri, zahati, maji yapo, ujenzi wa shule unaendelea na huduma nyingine nyingi zinaendelea kutekelezwa.
Hivyo, wananchi wameombwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kumpa kura zote za ndiyo Rais Mhe. Dkt. Samia, Mbunge Mhe. Simbachawene na Madiwani ili waenedelee kuijenga nchi kwa kasi.
Mhe. Simbachawene anaendelea na ziara yake katika Jimbo la Kibakwe ambapo amefanya mikutano ya hadhara katika Kijiji cha Muungano, Wiyenzele na Chipogolo katika kata ya Chipogolo, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
0 comments:
Post a Comment