CHAMA
cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha HAZINA SACCOS Ltd kimewezesha wanachama
wake (watumishi wa umma) kupata mikopo ya zaidi ya sh bil 100 tangu kuanzishwa
kwake.
Hayo
yamebainishwa leo na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Festo Mwaipaja alipokuwa
akizungumza na wanahabari kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD)
yanayofanyika Kitaifa Mjini Tabora.
Alisema
kuwa mfuko huo ulioanzishwa mwaka 1972 na kusajiliwa rasmi mwaka1973 ulilenga
kuhudumia watumishi wa Wizara ya Fedha pekee
lakini baadaye ukahusisha watumishi wa Wizara zote Tanzania Bara.
Alibainisha
kuwa chama hicho kilianza na wanachama 250 lakini kutokana na huduma yake nzuri
na manufaa makubwa wanayopata wanachama wake hadi sasa kimefikisha wanachama
8,000.
Mwaipaja
alibainisha kuwa hadi sasa chama kina akiba za wanachama za kiasi cha sh bil 29
ambazo zimetokana na michango yao na wanachama wote wameendelea kunufaika na
mikopo minono ya kimaendeleo.
‘Mfuko
huu ni mkombozi kwa watumishi wa umma wote Tanzania Bara kwa kuwa wanaruhusiwa
kuchukua kiasi chochote wanachotaka wakati wowote kwa utaratibu uliowekwa na
kurejesha pasipo usumbufu wowote, hadi sasa tumeshatoa mikopo ya zaidi ya sh
bil 100’, alisema.
Alifafanua kuwa wana mikopo isiyoangalia
akiba, inayoangalia akiba na ya ununuzi wa viwanja, na kupitia mikopo hiyo
wanachama wao wameendelea kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Mikopo
isiyoangalia akiba alisema kuwa ni ile ya kijamii ambayo ni dharura, elimu,
mazishi na sikukuu ambapo mwanachama anaweza kuchukua kati ya sh laki 5 hadi
mil 5 kulingana na hitaji lake.
Kwa
mikopo inayoangalia akiba alisema kuwa ni ile ya maendeleo, biashara, ujenzi na
hitaji maalumu (standing order) ambapo kiasi kinachotolewa ni kati ya sh mil 20
hadi 50.
Mtendaji
Mkuu alieleza malengo makuu ya taasisi hiyo kuwa ni kuinua maisha ya watumishi
wa umma na kuwawezesha kutatua changamoto yoyote ya kimaisha itakayotokea mbele
yake ili kukidhi mahitaji yao.
Aliongeza
kuwa mfuko huo unahudumia watumishi wa umma wa aina zote wakiwemo Viongozi
Wakubwa, hivyo akabainisha kuwa wako makini sana katika usimamizi wake, hakuna
ubabaishaji wa aina yoyote.
0 comments:
Post a Comment