Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amemuagiza Waziri wa
Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhakikisha anasimamia ujenzi wa barabara ya
Malagarasi - Ilunde - Uvinza (km 51.1) kwa kiwango cha lami ukamilike ifikapo
mwezi Machi, 2025.
Dkt. Mpango ametoa agizo
hilo leo Julai 8, 2024 katika eneo la Malagarasi wakati akikagua utekelezaji wa
mradi wa ujenzi wa barabara ya Malagarasi - Ilunde - Uvinza kwa kiwango cha
lami na kuridhishwa na maendeleo yake.
“Hii barabara imesuasua
sana hasa kipindi cha mvua, na huku Kigoma bado tunapata mvua nyingi kwa hiyo
Waziri tutumie kipindi hiki cha kiangazi kukimbiza hii barabara iishe kama ulivyoahidi
na sisi tupite hapa tukiwa tumevaa suti, Simamieni hili Waziri pamoja timu
yako”, ameeleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesema kuwa
wananchi wa Kigoma wameisubiria barabara ya Uvinza - Malagarasi kwa muda mrefu
na ni muda sasa ikamilike na wananchi waweze kuendelea kufanya biashara na
kukuza uchumi wa Mkoa.
Amesisitiza kuwa uwepo wa
miundombinu bora ya barabara kutaufanya Mkoa wa Kigoma kuwa Kitovu cha biashara
na Mikoa mingine pamoja na nchi za jirani na kuwezesha wawekezaji kufika na
kuwekeza katika Mkoa huo.
Dkt. Mpango ameagiza
Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha hawapotezi ubora na viwango
vilivyowekwa kwa mujibu wa Mkataba.
Kwa upande wake, Waziri
wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa kipindi cha nyuma mradi wa ujenzi
wa barabara ya Uvinza - Malagarasi ulikuwa una suasua hivyo Wizara ilichukua
hatua ya kumuondoa Mhandisi Mshauri na kuleta Mhandisi Mshauri mwingine na sasa
hivi ujenzi unaendelea vizuri.
Ameeleza kuwa baada ya
hatua hiyo utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo hivi sasa unafanyika usiku na
mchana na amemuahidi Makamu wa Rais kuisimamia barabara hiyo ikamilike kwa
mujibu wa mkataba ifikapo mwezi Machi, 2025.
Bashungwa ameongeza kuwa
hivi sasa kazi za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zinaendelea
kuunganisha Mkoa wa Kigoma na Katavi ambapo wakandarasi wawili wamegawanywa
katika barabara hiyo kwa vipande vya kilometa 25.
Akitoa taarifa ya mradi,
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta,
ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Uvinza - Malagarasi (km 51.1) umefikia
asilimia 54 na sasa hivi kazi zinafanyika usiku na mchana ili mradi huo
ukamilike kama ulivyopangwa.
Ameongeza kuwa
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Uvinza - Malagarasi
unatekekelezwa na Mkandarasi kampuni ya STECOL Corporation na Mhandisi Mshauri
Kampuni ya NORPLAN na unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 62.7.
0 comments:
Post a Comment