Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Suleiman
Serera kesho anatarajiwa kuikabidhi bendera na kuiaga timu ya Taifa
itakayoshiriki katika Michezo ya
Olimpiki ya Majira ya joto inayoanza
siku ya Ijumaa Julai 26 hadi Jumapili Agosti 11, 2024 jijini Paris na miji
mingine 16 nchini Ufaransa.
Makamu wa rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Henry Tandau amesema
hafla hiyo ya kukabidhi bendera na kuwaaga jumla ya wanamichezo 15
wataoiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo ya Olympiki mwaka huu, itafanyika
kuanzia saa tatu asubuhi katika Uwanja wa Benjamin William Mkapa jijini Dar es
salaam.
Tandau amesema katika toleo hili
la 33 la Michezo hiyo ya Olimpiki,
kikosi cha Tanzania kitakuwa na nahodha mkimbiaji Alphonce Felix Simbu ambaye
pamoja na mkimbiaji mwenzie Gabriel Geay
watashiriki katika mbio za Marathon kwa wanaume.
Ametaja wengine kuwa ni wanariadha
Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri, ambao watashiriki michuano ya Marathon kwa
wanawake.
Pia amewataja waogeleaji wawili,
Sophia Anisa Latiff atakayechuana mita 50 freestyle, kategoria ya wanawake na
Collins Phillip Saliboko atakayecheza mita 100 freestyle kwa wanaume.
Mwanamichezo wa saba ni Andrew Thomas Mlugu, atayeshiriki katika
mashindano ya mchezo wa Judo,
Tandau amesema timu hiyo itaambatana na makocha 3 wa fani hizo tatu za
michezo, daktari wa timu, Mwambata wa Mawasiliano na Habari pamoja na maafisa
wawili kutoka TOC.
Zaidi ya wanamichezo 10,500 kutoka mataifa 206 wanatarajiwa kushiriki
katika matukio 329, na fani 45 tofauti
za michezo. Kwa mara ya kwanza kila jinsia
itawakilishwa na wanamichezo 5,250.
Katika michezo hiyo kutakuwepo na
Breaking (aina ya breakdancing) ambayo itakuwa ikichezwa kwa mara ya kwanza
kwenye Olimpiki, pamoja na kuteleza kwa ubao (Skateboarding) kupanda ukuta na
kuelea kwenye mawimbi (surfing) makubwa
ya bahari.
Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki mwaka
1964 huko Tokyo, Japan, na toka wakati huo imepeleka wanariadha kushiriki katika kila
Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto isipokuwa ile iliyosusiwa mwaka
1976, ila haijawahi kushiriki Michezo ya
Olimpiki ya Majira ya baridi.
Mwaka huo wa 1976, nchi 29, nyingi zikiwa za Kiafrika, zilisusia Michezo
ya Olympic iliyofanyika Montreal, Canada, baada ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kukataa
kuipiga marufuku New Zealand, baada ya timu yake ya kitaifa ya raga
(rugby) kuzuru Afrika Kusini mapema
mwaka 1976 kinyume na wito wa Umoja wa Mataifa wa michezo ulioiwekea Afrika
Kusini vikwazo kutokana na msimamo wao wa ubaguzi wa rangi.
Kamati ya Taifa ya Olimpiki ya Tanzania iliundwa mwaka 1962, ili
kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Glasgow, Scotland. Mwaka 1968 TOC ilitambuliwa rasmi na Kamati ya Kimataifa
ya Olimpiki (IOC).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment